Kaunti zilizowalipa wauguzi kunyimwa pesa
Na ANGELA OKETCH
MWELEKEZI wa Bajeti, Agnes Odhiambo, ameonya Kaunti za Migori, Mombasa, Machakos na Kwale kwamba ni lazima zirejeshe pesa zilizolipa wauguzi kama marupurupu au zinyimwe pesa na Serikali ya Kitaifa.
Kaunti hizo hazikuathiriwa na mgomo wa wauguzi uliositishwa juzi kwa sababu zilikuwa zikiwalipa wauguzi marupurupu kufuatia mkataba wa pamoja wa 2017.
Hata hivyo, Bi Odhiambo aliandikia kaunti hizo barua kuzifahamishwa kwamba zilikuwa zikilipa marupurupu hayo kinyume cha sheria na kuzitaka zirejeshe pesa hizo.
Kwenye barua ya pili kwa kaunti hizo, Bi Odhiambo alisisitiza kuwa zikikosa kuthibitisha kuwa zimewakata wauguzi pesa hizo hazitapokea pesa kutoka Serikali ya Kitaifa.
“Serikali za Kaunti hazifai kulipa marupurupu ambayo hayajaidhinishwa na Tume ya Mishahara,” inasema barua kutoka kwa Bi Odhiambo.
Mwenyekiti wa Tume ya Mishahara, Lyn Mengich, alisema magavana na wizara ya fedha walithibitisha hawana pesa za kulipa wauguzi.
Chama wa wauguzi kinawataka magavana kutowadhulumu wauguzi kwa sababu wamerejea kazini.
Naibu Katibu Mkuu Maurice Opetu alimlaumu Bi Odhiambo kwa kuvuka mamlaka yake.
“Kwa nini Mwelekezi wa Bajeti anatisha serikali za Kaunti ambazo zinafaa kuwa huru. Wameacha jukumu lao la kuelekeza bajeti ya serikali ya kitaifa na sasa wanataka kuonyesha serikali za kaunti jinsi ya kusimamia bajeti,” alisema Bw Opetu.
Kulingana na Bw Opetu chama kimepokea ripoti kutoka kwa wauguzi Kaunti ya Narok kwamba gavana ametangaza kwamba atawafuta wote walioshiriki mgomo.
Mnamo Ijumaa, wauguzi walifutilia mbali mgomo baada ya kushinikizwa na serikali ya kitaifa na serikali za kaunti.