KBL yaondolea kampuni pinzani visiki vya usambazaji wa pombe
Na BERNARDINE MUTANU
KAMPUNI ya Kenya Breweries Limited (KBL) sasa iko huru kusambaza bidhaa zake za pombe hiyo sambamba na bidhaa za kampuni zingine za pombe.
Hii ni baada ya kampuni hiyo kuingia katika makubaliano na Shirika la Kudhibiti Ushindani (CAK) kuondoa baadhi ya matakwa kwa wasambazaji.
Kulingana na kandarasi, wasambazaji wa pombe ya KBL, tawi la EABL, hawakuwa na ruhusa ya kusambaza pombe ya washindani wa kampuni hiyo.
KBL ilibuni sera kuhusu ushindani itakayoiwezesha kuondoa sehemu tata za kandarasi kwa wasambazaji wake ambazo ziliwazuia kuuza kusambaza pombe nyingine isipo pombe za KBL.
KBL iliogopa ushindani sokoni kwa kuweka sehemu hiyo katika kandarasi zake na wasambazaji kulingana na utafiti wa CAK.
Sheria ya Ushindani imeipa CAK mamlaka ya kuipiga faini kampuni yoyote inayokiuka sheria hiyo hadi asilimia 10 ya mapato yake ya mwaka uliotangulia au inaweza kutoa agizo la kurekebishwa kwa miongozo na kanuni mbaya kwa upande wa kampuni.
Tofauti kati ya KBL na wasambazaji wake ziliibuka 2016 walipokataa kutia saini kandarasi kati yao na kampuni hiyo.