KCB kuokoa pesa za mlipa ushuru ikununua National Bank
Na BERNARDINE MUTANU
Benki ya National inatathmini ombi la Benki ya KCB la kutwaa usimamizi wa benki hiyo asilimia mia kwa mia.
Katika taarifa, NBK ilithibitisha kupokea ombi hilo, “Bodi ya kampuni itatathmini ofa hiyo kwa kina na kisha kujadiliana na kisha kutafuta idhini inayohitajika kutoka kwa washikadau na wadhibiti,” ilisema benki hiyo katika taarifa.
NBK ilipokea ombi hilo Aprili 18, 2019. Kulingana na taarifa hiyo, washikadau wakuu wameonyesha azma ya kutaka kuimarisha mtaji mkuu wa benki hiyo, “ambao unatarajiwa kuimarisha uwezo wa benki sokoni na huduma kwa wateja na ukuaji kwa ujumla.”
Benki hiyo ilisema itatangaza mapendekezo kuhusiana na ombi hilo kuambatana na sheria.
Hatua ya KCB itaifanya benki hiyo kuwa kubwa zaidi eneo hili. Benki hizo zimeorodheshwa katika Soko la Hisa la Nairobi.
Lakini biashara zao katika soko hilo zilisimamishwa Alhamisi asubuhi kutokana na tangazo hilo.
Benki ya NBK imekuwa ikishuhudia changamoto za kifedha na kumekuwa na habari kuhusiana na ununuzi huo katika muda wa miaka miwili sasa.
Ikiwa itanunuliwa na KCB, basi pesa za mlipa ushuru zilizowekezwa katika benki ya National, ambayo inashuhudia misukosuko ya kifedha, zitakuwa pahali salama.
“NSE ingependa kuwafahamisha wawekezaji, washikadau na umma kwamba tumesimamisha ununuzi na uuzaji wa hisa za KCB na NBK tungoja tangazo la rasilimali na NBK litakaloathiri meza hizo mbili,” NSE ilisema Alhamisi asubuhi.
NSE ilisimamisha biashara hiyo kuambatana na sheria zinazosimamia soko la hisa nchini.