KCB yaungana na benki ya Morocco kufanya biashara kimataifa
Na BERNARDINE MUTANU
Benki ya Kenya Commercial imetia saini mkataba na Benki ya Attijariwafa ya Morocco kwa lengo la kuimarisha biashara ya kimataifa.
Mkataba huo uliotiwa sahihi Casablanca, Morocco, unatarajiwa kuimarisha ushirika katika utoaji wa huduma bora zaidi katika benki, huduma za fedha ba biashara eneo la Africa Mashariki na Kaskazini Afrika.
Ushirikiana kati ya benki hizo utaendeshwa kupitia kwa mpango wa dijitali na simu za mkononi.
Hili litapelekea kuanzishwa kwa huduma za benki kwa niaba ya nyingine kwa lengo la kuwezesha operesheni za benki hizo na uhusiano wa kibiashara, alisema afisa mkuu wa operesheni wa KCB, Samuel Makome.
“Uhusiano huu utafaa sana sekta za muundo msingi na nyumba kupitia kwa miradi, kutoa msaada wa kiufundi na utoaji wa huduma bora. Benki zote mbili zitakubaliana kuhusiana na kiwango cha uwekezaji kinachohitajika kwa kila mradi,” alisema wakati wa mkutano wa kimataifa wa kimaendeleo Afrika wiki jana.
Mkutano huo ni sehemu ya misheni ya Attijariwafa ya kukuza uwekezaji kati ya benki za Afrika, biashara na ushirikiano.
Kutokana na hilo, nafasi mpya sokoni kwa wateja hasa mashirika ya humu nchini, biashara ndogo na miradi ya kina mama.
Benki hizo pia zitashirikiana kuhusiana na utoaji wa mafunzo na ajira.