• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
KCPE: Matokeo ya wanafunzi walemavu yaimarika

KCPE: Matokeo ya wanafunzi walemavu yaimarika

NA CECIL ODONGO

HUKU sherehe zikiendelea kunoga maeneo mbalimbali ya nchi baada ya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane(KCPE) kutolewa Jumatatu, walemavu pia hawajaachwa nyuma baada ya kung’aa kama wanafunzi wengine.

Kati ya wanafunzi 2,407 walemavu walioufanya mtihani huo, mwanafunzi wa kwanza alijizolea alama 414 huku wanafunzi 11 wakipata alama 400 na zaidi.

Matokeo hayo yalikuwa mazuri ikilinganishwa na yale ya 2018 ambapo walemavu wanne pekee ndio walikuwa na alama 400 na zaidi.

Wanafunzi 211 walipata kati ya alama 300 hadi 400, 726 wakapata alama 201-300, watahiniwa 1350 wakapata 101-200 na 45 pekee wakapata chini ya alama 400.

Idadi ya waliopata chini ya alama 100 pia ilipungua kutoka 76 mwaka jana hadi 45 mwaka huu.

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha jana alisema serikali itaendelea kutekeleza sera zitakazohakikisha wanafunzi walemavu wanapata elimu sawa na watoto wasiozaliwa na ulemavu wowote.

“Wizara ya elimu itaendelea kutekeleza sera ambazo zitahakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanasoma kama wanafunzi wengine,” akasema wakati wa kutangazwa kwa matokeo hayo katika jumba la Mtihani, jijini Nairobi.

Alifichua kwamba serikali inapanga kuzindua kituo cha kitaifa cha utafiti cha masomo ya saikolojia katika Taasisi ya Elimu(KISE) kwa watu wenye mahitaji maalum kuhakikisha wanafunzi walemavu wanasoma bila matatizo yoyote.

You can share this post!

KCPE: Wanafunzi kufahamu shule watakazojiunga nazo Desemba 2

KCPE: Shule za kibinafsi za wasichana zawika

adminleo