• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
KCPE: Shule za kibinafsi za wasichana zawika

KCPE: Shule za kibinafsi za wasichana zawika

Na WAANDISHI WETU

Shule ya kibinafsi ya High Vision iliwacha shule zinazoongoza za kibinafsi vinywa wazi baada ya kutoa mwanafunzi bora katika Ukanda wa Pwani katika mtihani wa kitaifa wa shule za msingi KCPE.

Rodney Isaack Kahura kutoka shule hiyo alitoka kidedea wa Ukanda wa Pwani baada ya kupata alama 431.

Pia iliyoshangaza ni Shule ya msingi ya kibinafsi ya Stone wall katika Kaunti ya Lamu baada ya kutoa mwanafunzi wa pili bora.

Aisha Haroon kutoka Kaunti ya Lamu aliyepata alama 429, Maku Hanifa Makena kutoka shule ya msingi ya Nyali kaunti ya Mombasa aliyepata alama 427.

“Hili ni jambo ambalo nimeshindwa kuamini japo nilifanya bidii sikutarajia kuwa mwanafunzi wa kwanza Ukanda wa pwani,nashukuru walimu wazazi na wanafunzi wenzangu kwa msaada na ushirikiano wao,” alisema Kahura akiongezea kuwa anatazamia kujiunga na shule ya wavulana ya Alliance ili kufanikisha ndoto yake ya kuwa mhandisi.

Mwengine kutoka shule ya Nyali Mombasa Khamis Hafidha Abdulaziz alipata alama 426.Mtihani huo pia pia ulioonyesha pengo katika shule ya serikali baada yao kushindwa kuorodhesha wanafunzi wao katika orodha ya wanafunzi 20 bora katika eneo la Pwani.

“Nafurahia kuongoza kaunti ya Lamu, shukrani zangu ni kwa Walimu wangu,wanafunzi na wazazi wangu waliyoshirikiana name kuona kuwa nimepata alama za juu,ndoto yangu ni kujiunga na shule ya upili ya wasichana ya Pangana na baadai kuwa mkunga,” akasema Aisha.

Katika shule ya msingi ya Nyali,Hafidha ambae ni mtoto wa msimamizi mkuu wa chuo cha kiufundi ya Mombasa (TUM)Laila Abubakar hakuweza kuficha furaha yake baada ya kugundua kuwa alikuwa watatu bora kataka ukanda wa Pwani.

Akizungumza na Taifa Leo katika shule hiyo,wasichana waliyoongoza eneo la Pwani walihusisha matokeo yao bora na bidii na kumuomba Mungu.

“Nafurahia kuongoza eneo la Pwani,ndoto yangu imetimia,haikuwa safari rahisi lakini kwa kuweka Mungu mbele nimefanikiwa,”akasema Hanifa aliyekuwa amejawa na furaha.Hanifa anapania kuwa dakitari baada ya kumaliza masomo yake ya shule ya upili.

“Nimefurahia mwanangu ameongoza ,niwaomba wasichana wengi kufanya bidii katika kila jambo wanalolifanya,” alisema Bi Halima Tsala mamake Hanifa.

Kwa upande wake Hafidha ambae alikuwa ameandamana na mamake Prof Abubakar aliwashukuru wazazi wake na walimu kwa kumuongoza muda wote katika masomo yake.Hafidha alisema anapania kuwa rubani baada ya kuhitumu masomo yake ya shule ya upili.

“Nafurahia kuona wasichana wanaongoza katika sehemu hii,tumefurahia matokeo bora,” alisema Prof Abubakar.

Mwalimu mkuu katika shule hiyo ya Nyali Bw John Kombo alisema alifurahia matokeo baada ya wanafunzi zaidi ya 27 kutoka shule hiyo kupata alama 400.

Katika shule ya kibinafsi ya Busy Bee kulikuwa na bwembwe na vifijo baada ya watahiniwa wao 36 walifanya mtihani huo kupata matokeo bora.

W akwanza aliyepata alama za juu zaidi ni Irene Muyaza aliyepata alama 422.

Mkuu wa shule hiyo Bi Dorothy Ndoro alisema matokeo hayo hayakuwashangaza kwani walitarajia kuwa wanafunzi wao wangefanya vyema.

“Tulitarajia matokeo bora kufuatia bidii na juhudi tulizotumia kuwatayarisha wanafunzi wetu,”akasema.

Katika Kaunti ya Kwale kulikuwa na vifijo katika shule ya Bethany Christian baada ya kutoa mwanafunzi bora katika katika mtihani wa KCPE.

Mwendwa Mwaniki, mwenye umri wa miaka 15, alipata alama 421. Alifurahia kupata matokeo hayo baada ya miaka minane ya juhudi na bidii katika masomo yake.

“Nashukuru Mungu kwa matokeo haya,nilifanya bidii kuhakikisha kuwa ninafaulu katika mitihani yangu,” alisema.

Mwaniki alifuatwa kwa karibu na Dorcas Ngowa aliyepata alama 417, anamatumaini ya kujiunga na shule ya upili ya Kenya.

Comfort Hiribae akiwa watatu na alama 415 na anatazamia kujiunga na shule ya upili ya Starehe.

Mkurugenzi wa shule hiyo Bw Young Lee alisema shule hiyo ilisajili wanafunzi 15 na wanane wa,mefanikiwa kupata alama 400.

Katika kaunti ya Tana river shule ya kibinafsi ya Life Frontier Madogo ambayo ilisajili wanafunzi 52 walifauli kutoa watano bora katika Kaunti hiyo.

Winnie Gloria Otieno alipata alama 413, akifuatwa na Alex Josephat Kyalo 404, na Mahabub Mohamed Said 402.

You can share this post!

KCPE: Matokeo ya wanafunzi walemavu yaimarika

KCPE: Nairobi yaongoza kwa waliofanyia mtihani gerezani

adminleo