Habari Mseto

KCSE: Walimu 900 wagomea usahihishaji

December 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WAANDISHI WETU

ZAIDI ya walimu 900 wanaosahihisha karatasi za somo la Biashara kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE), wamegoma kwa muda wa saa tatu wakilalamikia malipo duni.

Walimu hao ambao walikuwa wamekita kambi katika kituo cha usahihishaji cha Shule ya Wasichana ya Machakos, walikuwa wamelalamikia kulipwa Sh46 kwa kila karatasi wakitaka kiwango hicho kipandishwe hadi Sh68.

Kutokana na mgomo huo, Baraza la Kitaifa la Mtihani Nchini (KNEC) liliagiza kituo hicho kifungwe lakini likabadilisha uamuzi baadaye na kuafikiana na walimu hao kuongeza malipo yao hadi Sh52.

Walimu pia walikuwa wamelalamikia msongamano kwenye mabweni ya kulala.Suala hilo liliibua swali la iwapo wanafunzi watatendewa haki na ikiwa malalamishi kama hayo yameripotiwa kwenye vituo vingine vya usahihishaji lakini yakapuuzwa.

Ni kutokana na mgomo huo ambapo Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo (KUPPET) kiliitaka serikali kuimarisha mazingira ya walimu wanaosahihisha mtihani kwenye vituo vyote 20 jijini na viungani mwa Nairobi.

Katibu wa KUPPET, Akello Misori alishutumu Knec kwa kuwanyanyasa na kuwatumia walimu 26,000 wanaosahihisha mtihani huo vibaya kwa kuwalipa pesa kidogo.

“Ni jambo la kusikitisha kwamba walimu wanafanya kazi na kukesha kwenye mazingira mabovu. Tunalitaka baraza likome kuwatisha kuwafuta kazi wasahihishaji wa mtihani ambao wanalalamika,” akasema Bw Misori.

Kulingana na walimu wanaoshahihisha somo la Biashara, kiini cha malalamishi hayo ni ubaguzi dhidi yao ikizingatiwa wenzao wanaoshughulikia masomo ya Kingereza na Kiswahili wanalipwa Sh60 kwa kila karatasi.

“Tunaungana na walimu na tunataka malipo ya walimu wasahihishaji yaongezwe kwa asilimia 100 kwa kila karatasi. Walimu wamelazimika kutumia choo kimoja na bafu chafu, hali inayowaweka kwenye hatari ya kupata maradhi hatari,” akaongeza Bw Misori.

Akizungumza mjini Mombasa, Waziri wa Elimu Prof George Magoha alisema suala hilo limetatuliwa na walimu hao wanaendelea na usahihishaji.