• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
KDF wanatuhangaisha usiku,walia wakazi wa Mpeketoni

KDF wanatuhangaisha usiku,walia wakazi wa Mpeketoni

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa miji ya Mpeketoni, Hongwe na Kibaoni Kaunti ya Lamu wamelalamikia mateso wanayopitia mikononi mwa maafisa wa jeshi (KDF) wanaoshika doria eneo hilo hasa majira ya usiku.

Wakiongozwa na Mwakilishi wa Wadi ya Hongwe, James Komu, wakazi wamelalamika kwamba KDF wamekuwa wakiwapiga na kuwalazimisha kuogelea au kunywa maji chafu ya vidimbwi barabarani punde wanapowapata wakitembea barabarani usiku.

Bw Komu alimtaka waziri wa usalama wa ndani, Fred Matiang’i kuingilia kati na kukomesha madhila yanayoendelezwa na KDF dhidi ya wananchi wa Mpeketoni.

Pia aliitaka serikali kueleza waziwazi iwapo sheria ya kutotembea usiku almaarufu kafyu bado inaendelezwa eneo la Mpeketoni.

Mnamo Juni, 2014 siku chache baada ya Al-Shabaab kushambulia na kuua wakazi zaidi ya 100 mjini Mpeketoni, Kibaoni, Witu na Hindi, serikali iliamrisha kafyu kuendelezwa kwenye kaunti ya Lamu.

Mojawapo ya sehemu ya mji wa Mpeketoni. Wakazi wanadai KDF wamekuwa wakiwahangisha na kuwadhulumu usiku. Picha/ Kalume Kazungu

Sheria hiyo hata ghivyo iliondolewa tangu Oktoba, 2015 baada ya usalama kudhibitiwa Lamu.

Bw Komu alisema inashangaza kwamba wakazi wa Mpeketoni na sehemu zingine za Lamu bado wamekuwa wakinhyimwa uhuru wa kutembea.

“Ikifika saa mbili za usiku na ukiwa Mpeketoni, Kibaoni au Hongwe basi una kesi ya kujibu. Maafisa wa KDF wakikupata wanakupiga na kukudhalilisha. Wakazi hapa wamekuwa wakinilalamikia na lazima dhuluma hizo zikome.

Kwa nini watu wetu wanyimwe uhuru wa kutembea sehemu yao ilhali hakuna kafyu? Hatujaridhishwa na tabia za KDF na ningeomba Waziri Matiang’i achunguze na kukomesha visa hivyo hapa Mpeketoni. Tunaumia,” akasema Bw Komu.

Naye Simon Kimani alisema idadi kubwa ya wananchi wanalazimika kujikaza kubakia majumbani mwao kufikia saa kumi na mbili unusu jioni ili kuepuka kichapo kutoka kwa walinda usalama.

Kwa upande wake aidha, Msemaji wa KDF, David Obonyo alikana kuwepo kwa dhuluma zozote zinazoendelezwa na KDF dhidi ya wananchi wa Mpeketoni na Lamu kwa jumla.

Badala yake, Bw Obonyo alisema wamejitahidi kuendeleza ushirikiano bora na raia eneo hilo.

“Madai hayo si ya kweli. KDF hawawezi kudhulumu mwananchi bila sababu. Hiyo itakuwa ni kuzidisha ugumu wa kazi yetu. Jumatano tulikuwa na kikao na wananchi na hata viongozi eneo hilo na malalamishi yao yalikuwa ni kuhusu polisi. Wanadai polisi wanaitisha hongo kutoka kwa raia eneo hilo. Hakukuwa na malalamishi yoyote yaliyohusisha KDF,” akasema Bw Obonyo.

Aliwasihi wananchi kuendelea kushirikiana na walinda usalama eneo hilo ili kuhakikisha vita dhidi ya Al-Shabaab vinafaulu na Lamu isalie kuwa na amani.

You can share this post!

Vyuo vyatakiwa kubuni ofisi za kusaidia wanafunzi kuhusu...

Wakazi wafurahia biashara ya mafuta ndani ya Bahari Hindi

adminleo