Habari Mseto

KEBS kuhakikisha mafundi wametengeneza barakoa bora

April 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS) limetangaza kuwa litawasaidia mafundi kote nchini ili waweze kutengeneza maski zinazotimiza viwango hitajika.

Kwenye notisi iliyochapishwa kwenye gazeti la Daily Nation, toleo la Ijumaa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Benard Njiraini maafisa wake wameanza kuzunguka kote nchini wakiwaelekeza mafundi kuhusu namna ya kutengeneza maski hizo za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

“Maski zinazokubalika ni zile ambazo zimetengenezwa kwa vipande vya nguo vilivyotunganishwa mara tatu. Kitambaa cha kuzuia unyenyevu kinapasa kuwa katikati,” akasema.

“Na maski hizo zinaweza kutumika kwa mara kadhaa mradi zioshwe kwa sabani na maji,” akaongeza Bw Njiraini.

Hakikisho la KEBS limejiri baada ya Wizara ya Afya kutoa agizo kwamba sharti watu wavalie maski hizo katika maeneo ya umma nyakati zote

Kulingana na agizo hilo lililochapishwa kwenye toleo la hivi punde la gazeti rasmi la serikali, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe anasema wale ambao watakaidi agizo hilo na kanuni zingine za kupambana na Covid-19 watakamatwa na kuadhibiwa kwa faini ya Sh20,000 au kifungo cha miezi sita gerezani au adhabu zote mbili.

Serikali imekuwa ikihimiza kampuni za kutengeneza nguo na mafundi wa nguo kutengeneza vifaa hivyo kwa wingi ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Hii ni baada ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kutoa kuthibitisha kuwa kuvalia maski au barokoa ni njia mojawapo ya kuzuia watu kuambukizwa virusi hivyo ambavyo vinaweza kusalia hewa kwa zaidi ya saa tatu.

Wakati huo huo, Bw Njiraini aliwashauri Wakenya kutotumia maski za aina ya N95 ambazo hutumiwa na wahudumu wa afya pekee na wagonjwa.

Wiki iliyopita Waziri wa Biashara na Viwanda Betty Maina alitoa wito kwa mafundi na kampuni za humu nchini kama vile Rivatex (ya Eldoret) na Kicotec (ya Kitui) kuuza vifaa hivyo kwa bei nafuu.