• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Kenya imeoza, yataka mageuzi ya dharura – Mudavadi

Kenya imeoza, yataka mageuzi ya dharura – Mudavadi

Na CECIL ODONGO

KINARA wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi ameeleza masikitiko yake kuhusiana na jinsi hali ilivyo nchini.

Huku taifa hili likijiandaa kusherehekea Sikukuu ya Madaraka hapo Jumamosi, Bw Mudavadi alisema ni dhahiri wananchi hawajapata ukombozi waliotamani wakati Kenya ilipopata uhuru kutoka kwa mabeberu.

Kulingana naye, karibu kila sekta, kutoka kwa usalama, elimu na uchumi zinaendeshwa kwa njia inayoathiri vibaya maisha ya mwananchi wa kawaida na hivyo basi Rais Uhuru Kenyatta anahitaji kuwaza upya kuhusu jinsi anavyoendesha utawala huu.

Bw Mudavadi alikashifu serikali kwa kuendelea kukopa fedha kutoka mataifa ya kigeni, akidai pesa hizo huporwa na kumwachia mwananchi mzigo wa kutozwa ushuru wa juu ili kuyalipa madeni hayo.

Bw Mudavadi alisema Kenya huenda ikakosa kulipa madeni inayodaiwa na kujiweka pabaya machoni mwa jamii ya kimataifa huku akisisitiza kuwa serikali hukopa fedha na kuelekeza kwenye miradi bila utaratibu maalum wa kuhakikisha pesa hizo zinatumika vizuri.

“Kama kiongozi wa upinzani, nitaendelea kutumia vyombo vya habari kukemea mikopo ambayo hupandisha kiwango cha deni la taifa ilhali mwishowe huporwa na watu wachache. Serikali imeshindwa kubuni mbinu za kuhakikisha pesa zinazotengewa miradi lengwa zinapitia utaratibu ufaao badala ya kutolewa bila mpango,” akasema Bw Mudavadi kwenye kikao na wanahabari nyumbani kwake mtaa wa Riverside jijini Nairobi.

Matamashi ya naibu huyo wa zamani wa waziri mkuu yanakuja wiki chache baada ya Kenya kupokea mkopo wa Sh210milioni za Eurobond huku ikibainika kwamba Waziri wa Fedha Henry Rotich anatafuta mkopo mwingine wa Sh75 bilioni kugharimia utekelezaji wa Maazimio Manne Makuu ya serikali.

“Ufisadi unaoshuhudiwa nchini umefikia kiwango cha kutisha na sasa umegatuliwa hadi katika serikali za kaunti. Mawaziri na magavana wamekuwa wakifika kuhojiwa katika afisi za EACC (tume ya kupambana na Ufisadi) na DCI (Idara ya Upelelezi) na inasikitisha kwamba hakuna aliyehukumiwa hadi sasa,” akaongeza Bw Mudavadi aliyewahi kuhudumu kama makamu wa rais nchini.

Aidha, alishikilia kwamba chama cha ANC kiko tayari kuunga mkono au kadhamini mswada ambao utapendekeza mikakati ya kubuniwa kwa Mamlaka Huru ya Kudhibiti Deni la Taifa ambalo alisema linakaribia Sh6 trilioni.

Wakati uo huo, alipuuzilia mbali pendekezo la Kinara wa Upinzani Raila Odinga kwamba ngazi nyingine ya utawala inafaa kubuniwa, akisema tayari Wakenya wanakabiliwa na gharama kubwa ya kufadhili serikali za sasa.

“Huwa ninashangaa wakati baadhi ya viongozi wakuu wanapopendekeza tuongeze ngazi moja zaidi ya utawala. Kama kufadhili hizi za sasa ni vigumu itakuwaje tukiongeza nyingine? Viongozi wanafaa kuzungumzia mambo yanayowafaa raia badala ya kuwaongeza gharama zaidi,” akasema.

Mwanasiasa huyo alimwomba Rais Uhuru Kenyatta kusuluhisha utata unaoendelea kushuhudiwa kati ya viongozi wa Chama cha Walimu (KNUT) na Waziri wa Elimu George Magoha kuhusu utekelezaji wa mtaala wa Umilisi na Utendaji (CBC).

Uhusiano wa Kenya na mataifa jirani na ukosefu wa usalama katika maeneo mbalimbali nchini ni kati ya masuala mengine ambayo Bw Mudavadi aliomba serikali kuyaangazia.

You can share this post!

Kocha wa KNH alenga kushinda mechi zilizosalia na kumaliza...

Wiper yaanza mbinu za kumwadhibu Kibwana

adminleo