Kenya sasa yapokea barakoa zinazouzwa moja kwa Sh17,000
Na BRIAN AMBANI
WAHUDUMU wa afya watakuwa wa miongoni mwa watu wa kwanza humu nchini kutumia barakoa zilizotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa, ambazo zinagharimu maelfu ya fedha kila moja.
Hapa nchini, wananchi wengi wamezoea kutumia barakoa ambazo zinagharimu kati ya Sh10 hadi Sh100 pekee.
Hata hivyo, barakoa za kielektroniki ambazo zilitangazwa Jumanne nchini na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya LG zina uwezo wa kusafisha hewa wakati wa kupumua ili kukinga mtumiaji dhidi ya kuvuta hewa chafu, ikiwemo hewa iliyo na viini vya virusi vya corona.
Kampuni ya LG ilitoa msaada wa barakoa 300 aina ya PuriCare zitakazosambazwa kwa madaktari nchini kupitia kwa Muungano wahudumu wa Kimatibabu (KMA).
Kampuni hiyo ilitangaza kwamba zote ni za thamani ya Sh5 milioni kwa pamoja, ambayo inamaanisha kila barakoa ni takriban Sh17,000.
Hata hivyo, upekuzi wa Taifa Leo katika maduka ya mitandaoni ilibainisha kuna mataifa ambapo barakoa aina hiyo huuzwa hadi Sh30,000 kila moja.
Kampuni hiyo sasa inapanga kuanza kuuza barakoa hizo kote nchini mwaka 2021.
Mkurugenzi Mkuu wa LG Afrika Mashariki, Bw Sa Nyoung Kim alisema barakoa hizo zimeletwa wakati ambapo vita dhidi ya virusi vya corona vinashika kasi na watu wanahitaji magwanda ya kujilinda dhidi ya virusi hivyo.
“Barakoa za PuriCare zilitengenezwa ili kukidhi hitaji la vifaa ambavyo vinaweza kuwakinga watu dhidi ya virusi vya corona kote duniani. Barakoa hii inahakikisha kwamba anayeitumia anapumua vyema na kukingwa vizuri,” akasema.
Barakoa hizo ni za kipekee kwa kusafisha hewa inayoingia kwenye pua na ina betri ambayo hufanya kazi kwa muda wa saa nane kabla ya kuzima.
Kuna sehemu maalumu ya kuondoa hewa chafu mwilini mtu anapopumua, bila kuingiza uchafu kupitia sehemu hiyo.
Pia muundo wa barakoa hizo humpa anayezitumia nafasi ya kupumua bila tatizo lolote kwani kuna kidubwasha kinachohisi nguvu za mtu kupumua.
Kidubwasha hicho kitaongeza au kupunguza hewa inayoingia kwa msingi wa nguvu ambayo mtu anapumua nayo.
Kwa mfano, mtu anapoivaa akifanya mazoezi kama vile kukimbia, kiwango cha hewa inayoingia kitaongezeka kuliko kiwango cha mtu aliyekaa kwa utulivu.
Betri ya barakoa hizo huchukua muda wa saa mbili pekee kuchajiwa huku barakoa ikiwa na sehemu ya ndani ambayo inaweza kubadilishwa baada ya anayeivaa kuitumia kwa muda fulani.
Kutumika tena
Barakoa hizo pia zinaweza kusafishwa kisha kutumika tena.
Tayari zaidi ya wahudumu 1,500 wameambukizwa virusi vya corona wakiwa kazini.
Mara nyingi baadhi yao wamelazimika kuwahudumia wagonjwa wa Covid-19 bila kuvaa magwanda ya PPE ilhali wamekuwa mstari wa mbele kupambana na virusi hivyo.
Kulingana na KMA, karibu wahudumu 20 wamefariki baada ya kuugua virusi vya corona mwezi huu pekee huku ugonjwa huo ukiendelea kuenea nchini.
“Kukosekana kwa vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya kumekuwa changamoto kubwa kwa utoaji wa huduma hasa kwa madaktari na wahudumu kote nchini. Ingawa KMA inatambua uwezo wa watengenezaji bidhaa kote nchini wa kutengeneza barakoa, tunashukuru kampuni ya LG kwa kutoa barakoa hizi kwa wahudumu wetu wa afya wanaojali maslahi ya wagonjwa,” akasema Rais wa KMA, Dkt Were Onyino.