Habari Mseto

Kenya yapata mkopo mwingine kutoka Ufaransa

June 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Serikali imeongeza kiwango cha mkopo kufikia Sh2.54 trilioni baada ya kupewa mkopo wa Sh47 bilioni na Mamlaka ya Maendeleo ya Ufaransa (FDA).

Mkopo huo ulioidhinishwa na Mkurugenzi Mkuu wa FDA  Alhamisi utagharamia miradi ya uzalishaji wa kawi, maji, uchukuzi na usimamizi wa fedha za umma.

Shirika hilo liliingia katika mkataba na KenGen kufadhili uzalishaji wa kawi ya upepo Meru. KenGen ilipata Sh7 bilioni kufadhili ujenzi wa kiwanda hicho kitakachozalisha kawi ya uwezo wa 80 MW.

Kampuni ya kusambaza umeme(Ketraco) ilipata Sh10.9 bilioni ambazo zitatumiwa kujenga kituo kidogo Makindu na kituo cha kudhibiti shughuli cha kampuni hiyo.

Pia itafadhili mradi wa mfumo wa kusambaza stima wa Nairobi Ring. Mkurugenzi Mkuu pia alitia sahihi mkataba wa Sh14 bilioni kufadhili mradi wa Mwache, chini ya Bodi ya Maji ya Coast Water, kwa lengo la kumaliz upungufu wa maji Mombasa kwa kuongeza kiwango cha maji kinachotolewa kutoka lita milioni 50 kwa siku hadi lita milioni 190 kwa siku.

Kwa sasa, mji huo unahitaji lita milioni 150 za maji kila siku.