Habari Mseto

Kero la mafuriko Mai-Mahiu

April 25th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na ANTHONY OMUYA

Shughuli za usafiri zilitatizika kwa muda wa zaidi ya saa 10 Jumatatu usiku baada ya mvua ya mafuriko kunyesha.

Mvua iliyonyesha ilihribu sehemu ya barabara na kusababisha msongamano mkubwa wa magari. Picha/ Anthony Omuya

Wasafiri katika barabara ya Mai-mahiu – Nairobi na Narok walilala kwenye magari ya usafiri wa umma, kutokana na mvua nyingi ambayo ilikatiza uchukuzi.

Mvua hiyo hiyo iliyozua taharuki miongoni mwa wasafiri, iliathiri biashara nyingi na kusababisha maporomoko babarani.

Abiria wakesha barabarani katika eneo la Mai-mahiu. Picha/ Anthony Omuya

Baadhi ya mifugo  walisombwa kwa maji ya mvua na kuwaacha wakulima kwa hasara kuu hali ambayo iliacha vinywa wazi wasijue la kufanya.

“Hali hii imekuwa ikiendelea kwa muda baada ya mvua nyingi. Sio vyema kila siku mvua isababishe maafa ya mifugo na hasara. Suluhisho la kudumu linahitajika. Hii ni fedheha sana. Hasa kwa nchi yetu,” akasema mmoja wa wasafiri Ken Moimbo.

Ilibidi baadhi ya abiria washuke kwa gari na kujionea uharibifu uliosababishwa na mvua. Picha/ Anthony Omuya

Wasafiri wengi walilalamikia kile walichotaja kuwa kuzembea kwa  serikali hasa Wizara ya Uchukuzi.

Barabara iligeuka mto wa kuvuka. Picha/ Anthony Omuya

“Waziri anayehusika anafaa kuanzisha mikakati ya kumaliza tatizo la usafiri katika barabara hii wakati wa mvua, bidhaa nilizokuwa nikisafirisha kwa lori  za zaidi ya milioni tano sasa zimeharibika. Ni nani atanifidia ?” akasema Lucy Warimu, mwanabiashara wa mboga ambaye alikuwa akisafirisha bidhaa hizo jjijini Nairobi kutoka kaunti ya Bomet.

Wafanyakazi wa kukarabati barabara watazama kiwango cha uharibifu. Picha/ Antony Omuya

Wilson Chacha ambaye alikuwa akisafiri na wanawe watatu wa miaka mitano na kumi, alisema kuwa anahofia kwamba wanawe Huenda wakapatwa na kofu kutokana na baridi kali katika eneo hilo baada ya kulala kwenye basi walilokuwa wakisafiria kutoka Kisii.