• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Kero mama kujifungua karibu na lango la hospitali ya Pumwani

Kero mama kujifungua karibu na lango la hospitali ya Pumwani

Na SAMMY WAWERU

Hospitali ya kujifungulia kina mama ya Pumwani, Nairobi imemulikwa kwa mara nyingine kufuatia utepetevu wake katika utoaji wa huduma za uzazi.

Hii ni kutokana na video ya mama aliyejifungulia nje kwenye lango la hospitali hiyo ya uzazi.

Katika video hiyo ambayo haijulikani siku iliyonaswa, inayosambaa mitandaoni, mama huyo anaonekana akiteseka kujifungua bila usaidizi wowote wa wakunga au madaktari.

Kwenye video hiyo yenye matukio ya muda wa dakika 4 na sekunde 53, anaonekana akijifungua mtoto pembezoni mwa gari lililompeleka apate huduma za uzazi.

Adiha, wanaume kadhaa wanaokisiwa kumsafirisha wanaonekana wakihangaika. Ni hali ambayo inaalika watu, na chini ya dakika mbili hivi umati unafurika na kuanza kupiga nduru.

“Mtoto ashatoka…mtoto anatoka…” watu wanaskika wakipaaza sauti na kupiga kamsa. Kulingana na video hiyo, tukio hilo linaonekana kufanyika mita chache sana kutoka lango la Hospitali hiyo ya Pumwani, Nairobi ya kina mama kujifungua.

“Tusaidieni…” sauti za wanaume na wanawake zinaskika zikiomba msaada, katika muda wa dakika 1 na sekunde 41 wa video hiyo ya kuhuzunisha.

Wanaonekana wamevalia maski, ishara kuwa ni tukio lililofanyika kipindi hiki cha Homa ya virusi vya corona (Covid-19).

Kwa ghadhabu, wanasema madaktari wapo ila wanapuuza kuitika. Baadhi ya kina mama wanajitolea kumfunika kwa leso zao. “Chukueni mtoto…” sauti ya mwanamke inasema katika dakika ya 2 na sekunde 54.

Licha ya mbiu kuomba usaidizi kusaidia mama huyo kujifungua kupulizwa, kwa muda wa dakika 3 mfululizo hakuna mhudumu yeyote anayeonekana kujitokeza.

Mhudumu wa kike anaonekana kuanzia dakika ya 3 na sekunde 34. Isitoshe, kwa mujibu wa video hiyo, anasemekana kufika bila vifaa vya kazi. “Unakuja aje bila makasi?” anaulizwa.

Dakika ya 4 na sekunde 44, mama huyo anaoenakana akiingizwa hospitalini kwa kiti cha magurudumu, kinachotumiwa na wenye matatizo ya kutembea.

Ni utepetevu unaoghadhabisha waliofika kujaribu kumsaidia, kizaazaa kikichacha na watu wanatishia kutandika walinzi walio kwenye la Pumwani kwa kile wanadai ni kukataza mama huyo aingizwe hospitalini.

Kwenye mitandao ya kijamii, wachangiaji wameendelea kueleza ghadhabu na hasira zao wakitaka wasimamizi na wafanyakazi wa hospitali hiyo waadhibiwe kisheria.

“Mhudumu yeyote wa afya anayefanya kitendo cha aina hiyo (akimaanisha kupuuza mgonjwa), hapaswi kuwa kazini,” Makau Kioko ameeleza kwenye Facebook.

Irene Sandra Sandra anasema alitazama video hiyo mnamo Ijumaa Septemba 18, 2020, na anapendekeza wafanyakazi wote wa Pumwani watimuliwe kazini. “Natumai mama na mtoto aliyejifungua, wote wako salama. Wafanyakazi wote wa Pumwani watimuliwe au hospitali hiyo ifungwe,” Sandra akachapisha.

Si mara ya kwanza hospitali hiyo ya huduma za uzazi kumulikwa, kutokana na utepetevu wake. “Pumwani imeripotiwa na visa vingi vya utendakazi mbaya. Tukio la mama huyo ni ishara hakuna hatua inayochukuliwa. Suluhu ni moja tu; Wafanyakazi wote walioko wafutwe kazi wengine waajiriwe na wawe waadilifu,” akapendekeza Charlie Bin Charlie’s.

You can share this post!

DIGRII ZA MAJUTO: Vibarua licha ya kusoma

Ugaidi wafanya vijiji Lamu visalie mahame