Kero ya mbwa katika mitaa ya mabanda
Na SAMMY KIMATU
WAKAZI katika mitaa miwili ya mabanda katika Kaunti ya Nairobi wameiomba serikali ya Kaunti kuua mbwa zaidi ya 20 wanaorandaranda na kuwa kero kwao kwa kubweka ovyo hasa usiku na kwa kuwatishia usalama wao.
Mbwa hao wameripotiwa kurandaranda katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba na Mukuru-Hazina kwenye eneobunge la Starehe.
Mbwa hao waliwashambulia na kuwauma watu watatu mwaka 2018 walipopitia karibu na pahali mbwa walikuwa wamezalia.
“Kufikia sasa, watu watatu waliumwa na mbwa wakipitia karibu na pale mbwa walizalia. Wana kupe wengi na tunaogopa maradhi ya kuambukizwa ikiwa hawatapuliziwa dawa,” Bw Mickey Mrefu Matata akaambia Taifa Leo.
Inadaiwa mmoja wa wamiliki wa mbwa hao aliwaacha nyuma baada ya kukosana na mmiliki wa nyumba kuhusu kodi ya nyumba na akafurushwa.
Mbwa hao hupatikana katika eneo la Karanjo, uwanja wa kanisa la Capstone na kundi lingine katika Steji ya Kaiyaba mkabala wa barabara ya Enterprise.
Juhudi za Taifa Leo kuwasiliana na wasimamizi wa mitaa husika hazikufua dafu.