Habari Mseto

KESI YA MWILU: Mwanasheria wa Uingereza apigwa breki

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

MAJAJI watano wa Mahakama kuu wamemzuia mtaalam wa masuala ya kisheria kutoka Uingereza (QC) Profesa Khawar Qureshi kuongoza kesi aliyoshtakiwa naibu wa Jaji Mkuu (DCJ) Philomena Mbete Mwilu.

Prof Qureshi alipata kizingiti kikubwa kwa vile hana leseni ya kuendeleza kazi za uana sheria nchini Kenya kwa vile yeye ni mgeni.

“ Prof Qureshi hana cheti kilichoidhinishwa na chama cha wanasheria nchini (LSK) kumruhusu kufanya kazi za uwakili nchini,” wakili James Orengo aliwaambia majaji watano wanaosikiza kesi aliyowasilisha mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) dhidi ya Jaji Mwilu.

DPP amewasilisha ombi katika mahakama kuu akiomba majaji hao watano waamue ikiwa yeye (dpp) yuko na uwezo wa kumfungulia mashtaka jaji anayehudumu kabla ya kupokea idhini kutoka kwa tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama (JSC).

Punde tu naibu wa DPP Bi Dorcus Oduor kusimama na kutambua viongozi wa mashtaka katika kesi hiyo  dhidi ya Jaji Mwilu, Bw Orengo alisimama na kuwaambia majaji hao kuwa Prof Qureshi hajahitimu kutekeleza kazi ya wanasheria nchini.

“Prof Qureshi hajaidhinishwa na chama cha wanasheria nchini (LSK) kufanya kazi za uwakili nchini,” alisema Bw Orengo akiongeza , “ Kamwe hii korti haipasi kumruhusu kusema chochote mahakamani.”

Bw Orengo hakuna mwanasheria yeyote anaweza kukubaliwa   kumtetea mshukiwa nchini Uingereza bila kuidhinishwa na chama cha mawakili wa nchi hiyo ya ughaibuni.

Bw Orengo alisema Bi Oduor na naibu mwingine wa DPP Alexander Muteti na wakili wa Serikali Bw Emmanuel Mbita wanaweza kuendeleza kesi hiyo kwa vile wamehitimu ipasavyo.

Jitihada za Bi Oduor kuokoa dau la Prof Qureshi kuzama ziligonga mwamba.

Kuona mambo yamechacha , Bi Oduor aliomba mawkili Orengo na Okong’o Omugen ambao pia ni Maseneta na wabunge Daniel Maanzo , Peter Kaluma , Milly Odhiambo na Vincent Kemosi wazuiliwe kumwakilisha Jaji Mwilu akisema , “ DPP hufika mbele ya mabunge haya kuelezea utenda kazi wake.”

“ Wabunge hawa ndio wakuu wa DPP ambaye hufika kwao mara kwa mara kueleza utenda kazi wake. Naomba watimuliwe pia katika kesi hii.” Bi Oduor.

Wakitoa uamuzi majaji Hellen Omondi , Mumbi Ngugi , Francis Tuiyot , Chacha Mwita na William Musyoka walimtaka Prof Qureshi asite kuongoza kesi hiyo hadi kesi ya kumtimua itakapowasilishwa na kuamuliwa Janauri 19 2019.

Pia majaji hao waliamuru maombi mengine yawasilishwe na kuamuliwa wakati huo.

Jaji Mwilu aliwasilisha kesi akipinga kufunguliwa mashtaka akisema haki zake zimekandamizwa na idara ya mahakama inashambuliwa na afisi ya rais.