Habari Mseto

Khalwale akerwa na korti kutaja kesi dhidi yake mara 30 na kushindwa kuamua

September 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MTALAAMU wa kompyuta aliyeajiriwa na kampuni ya kusaga unga ya Shree Sai Millers Limited Jumanne alipinga kufunguliwa mashtaka katika mahakama ya Milimani akisema amehudhuria korti ya Kibera mara 30  na kesi dhidi yake ya wizi wa Sh32 milioni haijasikizwa.

“Mshtakiwa huyu ameenda mahakamani mara 30 na kesi dhidi yake haijasikizwa,” alisema wakili Wilberforce Khalwale.

Bw Khalwale alimweleza hakimu mkazi wa mahakama ya Milimani Bi Hellen Onkwani kuwa mahakama inasikitishwa na upande wa mashtaka ambao umeshindwa kuwawasilisha mashahidi katika kesi dhidi ya Bw Oscar Onganya.

“Mshtakiwa alitiwa nguvuni mnamo Desemba 24, 2013 na kushtakiwa kwa kosa la kuibia mwajiri wake Sh32 milioni,” alisema Bw Khalwale.

Hakimu alielezwa mshtakiwa alifikishwa mahakamani mnamo Desemba 30, 2013.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mshtakiwa amekuwa akihudhuria kesi na “haijwahianza kusikizwa tangu 2013.”

Korti ilijuzwa kuwa upande wa mashtaka haujakuwa ukiwasilisha mashahidi.

“Mahakama ya Kibera ilikuwa imeamuru upande wa mashtaka uwasilishe mashahidi kufikia Oktoba 29, 2018 na ikiwa hawatakuwa wamefanya hivyo kesi itatupwa,” alisema Bw Khalwale.

Alisema upande wa mashtaka ulimfungulia mashtaka mapya na kuyawasilisha katika mahakama ya Milimani Nairobi kwa vile korti imetoa vitisho kuzamisha kesi hiyo.

Bw Khalwale aliomba mahakama ikatae kumwuliza mshtakiwa ajibu mashtaka akiongeza kuna wafanyabiashara wawili walioweka mktaba na Shree Sai Millers kulipa pesa hizo.

Hakimu alifahamishwa kuwa Mabw Josphat Ng’ang’a na Karigithe Theuri walitia saini mkataba watalipa Shree Sai Millers pesa hizo.

Bi Onkwani aliamuru mshtakiwa azuiliwe hadi Jumatatu ndipo aamue ikiwa kesi itarudishwa Kibera ama itasikizwa Milimani.