KICD motoni kwa kusambazia wanafunzi viziwi vitabu vya Kifaransa
TAASISI ya Kuandaa Mtaala Nchini (KICD) imepigwa darubini kutokana na hitilafu katika usambazaji vifaa vya masomo baada ya kubainika ilituma nakala za vitabu vya lugha ya Kifaransa kwa shule zisizofundisha lugha hiyo ya kigeni.
Kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathugu, miongoni mwa shule zilizopokea vitabu hivyo, ambavyo havihitaji, ni shule za watoto wenye ulemavu wa kuona na kusikia, hali iliyochangia ubadhirifu kwa rasilimali za umma.
“Katika mwaka ambapo uchunguzi ulifanywa, kampuni moja ya uchapishaji ilipewa zabuni ya kuwasilisha nakala milioni moja ya vitabu vya kiada vya somo la Kifaransa vya wanafunzi wa Gredi ya Saba.
Hata hivyo, ukaguzi uliofanywa Januari 2024 ulionyesha ni shule moja tu katika Kaunti za Nakuru, Bungoma na Kakamega hufundisha somo la lugha ya Kifaransa.
“Vile vile, Shule ya msingi ya walio na ulemavu wa kusikia za Kwale na ile ya ‘Salvation Army’ Likoni ya wenye ulemavu wa kuona zilipokea nakala za vitabu vya kiada vya somo la Kifaransa ambavyo haziwezi kutumia. Katika hali hiyo, thamani ya pesa ilipotea kupitia ununuzi wa vitabu zaidi na kutoandaliwa kwa vitabu vinavyoweza kutumika katika shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum,” inasema ripoti hiyo.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaipongeza KICD kwa kupitisha kiwango hitajika cha ukusanyaji mapato kwa kima cha asilimia 65.