Kieleweke wadai Ruto alimchokoza Rais ndipo akazomewa hadharani
Na NDUNGU GACHANE
WANACHAMA wa Jubilee wanaopinga kampeni za mapema za Naibu Rais William Ruto wamedai matamshi ya Rais Uhuru Kenyatta aliyotoa Jumapili yalisababishwa na jinsi naibu wake na wandani wake wamekuwa wakimkaidi kuhusu handisheki na kampeni za mapema.
Viongozi hao walio katika makundi ya Kieleweke na Team Embrace wanaotetea misimamo ya Rais, walidai kuwa hakuna uhusiano mwema kati ya viongozi hao wawili wakuu baada ya Ruto kumkaidi Rais Kenyatta kuhusu malengo ya amani na umoja wa taifa.
Mnamo Jumapili, Rais aliongea kwa ukali akisema hakuna chochote kitamzuia kutafuta umoja wa makabila yote nchini.
Matamshi hayo yalionekana kulenga wanaopinga muafaka wake na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga ambao huwa wanadai waziri huyo mkuu wa zamani ni tapeli aliye na nia ya kuvuruga Jubilee.
Viongozi wa Kieleweke wakiongozwa na mbunge wa Gatanga, Bw Nduati Ngugi, Kabando wa Kabando na wenzao wa Team Embrace wakiwemo Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a, Bi Sabina Chege na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Beatrice Elachi, walikashifu wenzao wa Tangatanga kwa kumkosea Rais heshima.
“Rais amewasilisha ujumbe kwa Dkt Ruto na wafuasi wake kwa hivyo wasisubiri ishara nyingine yoyote. Wakomeshe kampeni zao na kutangatanga nchini na badala yake wafanyie kazi wananchi kabla Rais aanze kufanya ziara Mlima Kenya ikiwa wanataka kuokoa nyadhifa zao,” akasema Bw Ngugi.
Idadi kubwa ya viongozi wa kikundi cha Tangatanga hutoka maeneo ya Mlima Kenya na hudai kwamba Rais ametelekeza eneo hilo kimaendeleo.
Kwa upande wake, Bw Kabando alimkashifu Dkt Ruto kwa kufanya kampeni za mapema na kuchochea wananchi eneo la kati kumchukia Bw Odinga ilhali Rais analenga kuacha nchi ikiwa na umoja wakati atakapoondoka mamlakani mwaka wa 2022.
“Unapinga handsheki, juhudi za upatanisho na vita dhidi ya ufisadi kisha bado unadai kuwa mwaminifu kwa mkubwa wako?” akashangaa.
Alikosoa pia ziara iliyofanywa na naibu rais hivi majuzi eneo la Mukurweini ambapo wakazi walifika kutoka Karatina wakiwa wamevaa fulana zenye maandishi ya ‘WSR 2022’ na ‘Hustler Nation’, akasema hatua hizo zinafanya kuwe na taharuki za kisiasa ilhali uchaguzi ungali mbali.
Lakini viongozi wanaomuunga mkono Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya wakiongozwa na wabunge Kimani Ichungwa (Kikuyu) na Alice Wahome (Kandara) walilalamika kuhusu matamshi ya Rais wakisema ni dharau na kukosea heshima viongozi.
Wawili hao waliozungumza kwenye runinga tofauti walisema waliwachagua Rais Kenyatta na Dkt Ruto kwa pamoja na hivyo hawaoni tatizo kuandamana naye anapozuru maeneo tofauti ya nchi kufanya kazi.
“Haiwezekani kwamba wakati Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Amani National Congress Musalia Mudavadi na Bw Odinga wanapozungumza kuhusu siasa hakuna tatizo ilhali Dkt Ruto anapozunguka nchini kuzindua miradi inakuwa ni siasa,” akasema Ichungwa.
Kwa upande wake, Bi Wahome alisema: “Kutuita wakora ni sawa na kutupiga rungu. Hafai kusema hatukumsaidia kupata kura za urais. Tumekuwa tukipitisha miswada yote ya serikali bungeni.”