• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 1:36 PM
Kijana ‘fupi nono round’ amshtaki naibu gavana

Kijana ‘fupi nono round’ amshtaki naibu gavana

Na SAMWEL OWINO

MKAZI mmoja wa Pokot Magharibi amewasilisha ombi katika Seneti ili imchunguze Naibu Gavana Nicholas Owon Atudonyang, kwa kuendelea kuishi Amerika tangu alipoteuliwa, licha ya kupokea mshahara wa wadhifa huo.

Bw Dennis Ruto anayejulikana maarufu kama ‘Mulmulwas’, alisema Bw Atudonyang alichukua mkopo wa kununua gari na nyumba ya kifahari kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Pokot Magharibi, lakini amekuwa nje kwa muda mrefu bila kufanya kazi yake.

Bw Ruto anataka Seneti imchukulie hatua za kisheria Bw Atudonyang kwa kuvunja ahadi aliyoweka baina yake na wakazi wa Pokot Magharibi.

Ameambia kamati ya seneti kuhusu ugatuzi na mahusiano ya serikali kuwa mwenendo wa afisa huyo wa serikali umekiuka makubaliano yaliyowekwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017.

Anaitaka kamati hiyo kuingilia kati na kudadisi kwa nini afisa ambaye hafanyi kazi yake anaendelea kupokea mshahara na marupurupu, pesa ambazo ni za walipa ushuru.

Bw Ruto anasema kuwa naibu huyo wa gavana alirejea mwaka uliopita kutoka Marekani ili kushughulikia jambo la kibinafsi katika eneo la Kitengela.

“Hajawai kufika West Pokot, yeye huja kushughulikia mambo ya kibinafsi na kisha kuondoka,” akaeleza.

Aliongeza kuwa Bw Atudonyang ni daktari wa upasuaji Texas, Marekani na baada ya uchaguzi wa 2017 amekuwa akipokea mshahara wake licha ya kukosa kufanya kazi aliyochaguliwa kuifanya.

Bw Ruto, hata hivyo alipuuzilia mbali madai ya Gavana John Lonyangapuo aliyesema hapo awali kuwa naibu wake hasababishi hasara yoyote kwa kaunti hiyo kwani alishatolewa kwenye orodha ya wafanyakazi wa Kaunti ya Pokot Magharibi.

“Hata ingawa gavana anasema kuwa mshahara wa naibu wake ulisimamishwa, ni kweli Serikali ya Pokot inazidi kumlipia deni la mkopo aliouchukua kwa ajili ya kununua nyumba na gari,” akaambia kamati hiyo inayoongozwa na Senata wa Laikipia John Kinyua.

Alisema ataipa kamati hiyo anwani ya makazi anayoishi na kufanyia kazi naibu huyo wa gavana ili kuisaidia kwenye uchunguzi wake. Aliongeza kuwa Bw Atudonyang anapokea mshahara mzuri kuliko ule ambao serikali ya kaunti inampa.

“Tulipolalamika kuhusu kutoonekana kwake, tuliambiwa kuwa alikuwa ameenda kutafuta vifaa vya matibabu. Miaka miwili imepita sasa na hata vile vyombo vya dawa vilivyoahidiwa havijafika huku,” akasema.

You can share this post!

Kibwana akana madai ya kufanyia kazi Tangatanga

Mbunge hatarini kupoteza kiti kwa kupigia Ruto debe

adminleo