• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Kijana wa miaka 21 kunyongwa kwa kuiba Sh200

Kijana wa miaka 21 kunyongwa kwa kuiba Sh200

Na BENSON MATHEKA

MWANAMUME mwenye umri wa miaka 21, Jumatano alihukumiwa kunyongwa kwa kutumia nguvu kumnyang’anya mwanamke kibeti chake na mali ya thamani ya Sh200.

Hakimu Mkuu Mkazi wa Kibera Faith Mutuku alipata John Oshea Kiplangat na hatia ya kunyang’anya Gladys Jerotich kibeti chake akimtisha kwa bastola bandia miaka miwili iliyopita.

Akimhukumu, Bi Mutuku alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kikamilifu kwamba Oshea alitisha kumjeruhi mlalamishi ambaye ni mwalimu wa shule ya Jimcy, Nairobi.

Mshtakiwa alimatwa na umma dakika chache baada ya kumvamia Bi Jerotich katika mtaa wa Dam eneo la Lang’ata jijini Nairobi mnamo Januari 28 2016.

“Mashahidi walikuona ukitenda kosa na walifika kortini kutoa ushahidi. Walikukamata na ulikuwa na bastola bandia ambayo ulitisha kutumia kumjeruhi mlalamishi,” alisema hakimu.

“Adhabu ya kosa la wizi wa mabavu ni kunyongwa. Unaweza kukata rufaa katika muda wa siku 14 iwapo hautaridhika na uamuzi huu,” hakimu alisema.

Katika ushahidi wake, mlalamishi aliambia mahakama iliambiwa kwamba alivamiwa na vijana wawili nje ya mtaa wa Dam alipokuwa akitoka kazini.

Alisema walimtisha kwa kifaa kilichofanana na bastola na mmoja akanyakua kibeti chake na kuanza kukimbia. Mwanamume aliyekuwa akipitia aliwakimbiza vijana hao akipiga kamsa.

Alivutia watu wengine ambao walimkamata mshtakiwa na kumpa kichapo kabla ya kumpeleka kituo cha polisi cha Lang’ata ambapo baada ya uchunguzi alifunguliwa shtaka la wizi wa mabavu.

Kesi iliendelea kwa miaka miwili hadi juzi alipopatikana na hatia na kuhukumiwa jana kunyongwa.

You can share this post!

Kalonzo, Mudavadi na Weta wapinga kubuniwa kwa jopo la...

SAKATA YA NYS: Washukiwa 24 kusalia ndani kwa siku 7

adminleo