Kimani Ngunjiri amkejeli gavana kwa kutelekeza watoto
NA RICHARD MAOSI
MBUNGE wa Bahati Kimani Ngunjiri amemshtumu gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui kwa ‘kuwatupa’ zaidi ya watoto 41, katika eneo la Torongo, Baringo.
Alimkejleli gavana huyo katika makao ya kurekebisha tabia (Jomec Rehabilitation and Empowerment Centre Nakuru) ambapo aliwapa watoto hao msaada wa chakula, mavazi na nguo.
Jomec ilichukua jukumu la kuwatunza baadhi yao baada ya kuguswa na matatizo yaliyowakumba wakiwa Torongo kwa mujibu wa vyombo vya habari
Ngunjiri alimtaka Gavana Lee kujisafishia jina mbele ya umma na kuomba msamaha,badala ya kubakia kimya, licha ya unyama aliotendea watoto wa mitaani,ikiaminika huenda jambo hili limekuwa likitendeka kwa muda tangu achukue usukani.
AIdha aliwakilisha stakabadhi mbili, moja kutoka kwenye mtandao wa WhatsApp na nyingine kutoka kwa vyombo vya habari kuonyesha kuwa serikali ya kaunti ilichangia kuwafurusha mjini,
Wakishirikiana na mbunge wa zamani wa Naivasha John Mututho,waliahidi kuanzisha uchunguzi na kufichua mengine ambayo yamebakia kuwa siri.
“Nimepata nakala ya barua kutoka katika serikali ya kaunti inayodai kuwa asilimia 70 ya chokoraa wanatoka katika kaunti jirani ila sio wakazi wa Nakuru, lakini huo ni uongo mtupu,”alisema.
Ngunjiri alieleza kuwa hakupendezwa namna ambavyo watoto hao walikabiliwa muda wa kutimuliwa .
“Huenda jamii ingehusishwa kabla ya kuchukua hatua kama hii,” aliongezea.
Kulingana naye Lee angefanya utafiti kabla ya kuwatupa kwa sababu wengi wao walikuwa ni mayatima.
Kwa upande mwingine BW Mututho alimsifia Ngunjiri kwa kuonyesha moyo wa utu kwa wasiojiweza katika jamii.
Hili linajiri siku chache baada ya watoto zaidi ya arubaini kupatikana katika eneo la Torongo kaunti ya Baringo wiki iliyopita.
Jomec ni kituo cha kurekebisha tabia,na kufikia sasa ndio kimbilio kwa watoto 36 waliopatikana huku watano kati yao wasijulikane waliko.
Kaunti ya Nakuru imekuwa ikishuhudia visa vingi vya uhalifu na utovu wa usalama hasa uuzaji wa mali ya wizi na bidhaa bandia.
Maeneo yaliyotajwa ni pamoja na barabara ya Mburu Gichua,daraja ya kuelekea katika hospitali ya Rufaa ya Nakuru na PGH Annex.