Habari Mseto

Kina mama walevi watia wakazi hofu

July 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WAIKWA MAINA

MAAFISA wa watoto na wenyeji wa kaunti ya Nyandarua wamejawa na wasiwasi kufuatia ongezeko la akina mama wanaotelekeza watoto na kwenda kushiriki ulevi.

Maeneobunge ya Ol Kalou na Kinangop yanaongoza kwa idadi ya akina mama wanaopuuza watoto, unajisi na maovu mengine yanayohusishwa na matumizi ya vileo.

Katika eneobunge la Ol Kalou, maafisa wa watoto wanasema watoto 35 waliokolewa katika muda wa miezi miwili baada ya kutelekezwa.

Katika kisa cha hivi punde katika mtaa wa Vatican, Jumatano jioni, wakazi wakiongozwa na afisa wa watoto wa Ol Kalou, Mary Gitonga walimuokoa msichana mwenye umri wa miaka mitano aliyeachwa na mama yake ndani ya nyumba ya kukodisha kwa wiki tatu.

Mkazi Martha Wairimu alisema mama ya mtoto huyo aliyetambuliwa kama Bi Peris Wanjiku Ndatha alikodisha chumba mwezi jana kisha akaondoka nyumbani wiki tatu zilizopita na hakurudi.

“Nasikia huwa anaonekana katika baa kuanzia usiku wa manane lakini haonekani mchana. Hatujui anakoshinda mchana. Alidanganya landilodi kuwa anatoka Nairobi lakini tumegundua anatoka kaunti ya Murang’a,” alisema Bi Wairimu, ambaye amekuwa akimtunza mtoto huyo.

Msichana huyo aliyeachwa alienda katika nyumba ya Bi Wairimu akilia kwa sababu ya njaa na kusema mama yake hakuwa amerudi nyumbani kwa siku mbili. “Alikuwa na njaa na mchafu,” alieleza.