Kinara wa NSSF taabani kujitaja mmiliki wa shamba la ekari 134
Na RICHARD MUNGUTI
ALIYEKUWA meneja mkuu hazina ya malipo ya uzeeni (NSSF) Josphert Konzolo alijipata taabani kwa kudai ndiye mmiliki wa shamba la ekari 134 lenye thamani ya Sh8bilioni.
Bw Konzolo aliyemweleza Jaji Elijah Obaga kuwa aliinunua shamba hilo kwa bei ya Sh96milioni alijikuta katika hali ya suinto fahamu.
Bw Konzolo alisema aliuziwa shamba hilo na Bw John Mugo Kamau kati ya 1998 na 2011.
“Nilinunua shamba hili kutoka kwa muwekezaji Bw Kamau kwa bei ya Sh96milioni kisha akanipa hati ya umiliki, “ Bw Konzolo alisema
Aliongeza alisaidiwa na mkewe marehemu Noel kulipia pesa hizo kupitia kwa kampuni ya mawakili ya Bw Macmillan Mutinda Mutiso.
Bw Konzolo alisema baada ya kununua shamba hilo liliandikishwa kwa jina la kampuni yao Telesource .Com Limited
Kinara huyo wa zamani wa NSSF alihojiwa kwa undani zaidi jinsi alivyonunua shamba hilo na wakili Cecil Miller anayewakilisha kampuni ya Muchanga Investments Limited ambayo wamiliki wake ni mfanyabiashara mwendazake Horatius Da Gama Rose na aliyekuwa makamu wa rais Moody Awori.
“Ulikuwa kinara wa NSSF?” Bw Miller alimwuliza Konzolo
“ Ndio,” alijibu
“Hebu mweleze Jaji Obaga ikiwa ulishtakiwa kwa ufisadi ukiwa kinara wa NSSF,” Bw Miller akasema.
“Ndio nilishtakiwa,” alijibu Konzolo na kumataka Bw Miller aeleze jinsi kesi ilivyokamilishwa.
“Hebu eleza korti kama nilifungwa ama kuachiliwa,” Konzolo akasema.
“Je ulishtakiwa kwa wizi wa Sh100 milioni kutoka kwa benki ya Barclays?” Miller akamuuliza.
“Ndio nilishtakiwa na nikaachiliwa. Kesi ilitokana na fitina tu za kikazi,”alijibu.
“Kisha nataka uieleza hii mahakama kwamba wewe na wakili wako Mutinda Mutiso mlishtakiwa kwa ulaghai wa shamba hilo pamoja na aliyekuwa waziri wa ardhi Charity Ngilu, “ Bw Miller alimwuliza tena.
Mlalamishiu huyo kwa gadhabu alimwuliza jaji amtetee kwa vile maswali anayoulizwa na Miller yanalenga kumharibia sifa
“Jibu maswali jinsi unavyoulizwa,” Jaji Obaga alimwamuru.
“Ndio nilishtakiwa pamoja na Bi Ngilu ambaye sasa ni Gavana wa kaunti ya Kitui,” akasema Konzolo
“Je unajua mliachiliwa na mahakama ya rufaa kwa vile tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC haikuwa na makamishna wa kutosha na sasa wapo na mnaweza kufunguliwa mashtaka tena,”alisema Bw Miller
Bw Konzolo alijibu na kusema maswali hayo yanalenga kushusja hadi yake katika jamii na kumfanya aonekane kama mtu mfisadi.
Bw Miller aliambia Mahakam kuwa ushahidi ulio na EACC na Mwanasheria mkuu unaonyesha kuwa nakala ya ufisadi aliyonayo Konzolo imepatikana kwa njia ya ufisadi. Kesi inaendelea