Habari MsetoSiasa

Kiranja wa Wengi Machakos atimuliwa kwa kukosa nidhamu

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA LILLIAN MUTAVI

Nafasi ya Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Machakos Bw Tariq Mulatya imechukuliwa na diwani mwingine.

Diwani huyo wa Masinga ya Kati aling’atuliwa mamlakni kwa utovu wa nidhamu na kupuuza uongozi wa chama cha Wiper.

Spika wa bunge hilo Florence Mwangangi alisema kwamba alipokea barua nne zikipendekeza kutolewa kwa Bw Mulatya kwa kukosa heshima bungeni na kudharau uongozi wa chama.

Nafasi ya Bw Mulatya ilichukuliwa na Moses Mitaa ambaye ni diwani wa Kangundo ya Kati.

“Nilipokea barua kutoka kwa muungano wa Nasa Mei 25, 2020 na barua nyingine kutoka kwa chama cha Wiper wakiomba kutolewa kwa Bw Mulatya,” alisema Bi Mwangangi.

Bw Mulatya alijiuzulu hapoJuni 8, akisema alifanya hivyo ili kuleta amani katika chama chake.

“Cha maana sasa ni kuwatumikia wananchi wa Masinga ya Kati walionichagua na kuhakikisha wampata maendeleo kutoka kwa kaunti,” ilisoma barua yake ya kujiuzulu.

Bi Mwangangi alisema kwamba kutolewa kwa Bw Mulatya kulianza kabla ya barua yake ya kujiziuzulu.

Wakati huo chama cha wiper kilitoa madiwani wengine kutoka kwa kamati za bunge. Bi Mwangangi alisema kuwa viti hivyo vitajazwa ndani ya kwa muda wa siku 14.