Kitendawili DNA ya mwili uliodhaniwa ni wa MCA aliyetoweka ikisema siye
MAAFISA wa polisi wanaendelea kufuatilia kifo cha diwani wa wadi ya Wajir Yusuf Hussein Ahmed baada ya uchunguzi wa DNA uliofanywa kwa mwili uliookotwa kutoka ziwa moja kukosa kuthibitisha kuwa ni yeye.
Familia ya diwani huyo ilikubali kufanyiwa uchunguzi wa DNA kwenye mwili uliookotwa kutoka Ziwa Yahud, takriban kilomita nane kutoka mji wa Wajir.
Katika matokeo yaliyotolewa Jumatano, familia ilitangaza kuwa mwili huo si wa jamaa yao.
Madaktari wawili walihusika katika uchunguzi huo; daktari wa kibinafsi aliyeajiriwa na familia na daktari wa serikali.
Kwa mujibu wa familia, daktari wao wa kibinafsi alithibitisha kuwa mwili huo si wa diwani huyo aliyetoweka.
Madaktari hao walichukua sampuli kutoka kwa mamake mwathiriwa, kaka zake wawili, na tishu za mwili zilizohifadhiwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Wajir.
“Matokeo yanaonyesha kuwa mwili si wa diwani aliyepotea. Vipimo vya DNA kati ya ndugu hao wawili na mama yao vilikuwa sahihi kwa asilimia 99, hivyo kuthibitisha uhusiano wao,” akasema daktari.
Mwili ambao haujatambuliwa katika hifadhi ya maiti ya Wajir una urefu wa 6’2″ na asili ya Kisomali.
Hakuna sehemu za mwili zilizokatwa kulingana na daktari.
Chanzo cha kifo kilibainika kuwa jeraha usoni.
Ripoti za kutoweka kwa diwani huyo zilizua hofu huku wenyeji wakiandamana dhidi ya mashirika ya usalama katika kaunti hiyo.
Hapo awali, familia hiyo ilifichulia Taifa Leo kwamba diwani aliyetekwa nyara alikuwa ameitwa na Kamati ya Usalama na Ujasusi ya Kaunti ya Wajir (CSIC) inayoongozwa na Bw Karuku Ngumo, Kamishna wa Kaunti hiyo.
Bw Ngumo tangu wakati huo amekana hayo licha ya barua aliyotia saini mnamo Agosti 6, 2024 akiomba diwani huyo afike mbele yao mnamo Agosti 6, 2024, kujadili “masuala yanayohusu usalama.”
Mnamo Septemba 13, Bw Hussein alitekwa nyara Nairobi akiwa kwenye teksi.