Habari Mseto

Kitui yafaulu kushona sare za machifu wote nchini

August 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KITAVI MUTUA

KAUNTI ya Kitui Jumatano iliwasilisha kifurushi cha kwanza cha sare za machifu na manaibu wao kwa Afisi ya Rais huku kiwanda chake cha kutengeneza nguo, kilichofunguliwa mwaka jana, kikianza kuandikisha ufanisi.

Yakiwa na lebo yenye maneno “Made in Kitui” (Imetengenezwa Kitui), mavazi hayo yaliyoshonwa katika kiwanda cha Kitui County Textile Centre (Kicotec), yalipokewa na kundi la maafisa wa serikali wakiongozwa na msaidizi wa Inspekta Jenerali wa Polisi, Musa Kakawa.

Sare hizo ziliagizwa na Serikali ya Kitaifa kufuatia amri iliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Aprili mwaka huu kama sehemu ya mpango wa serikali wa kuhimiza ununuzi wa bidhaa zinazotengenezwa humu nchini.

Gavana wa Kitui, Bi Charity Ngilu alisema anafurahi kwamba kiwanda hicho kinachomilikiwa na serikali yake, kimeweza kutekeleza kibarua cha kutengeneza sare za maafisa wa utawala kwa muda wa miezi mitatu pekee.

“Leo (Jumatano) ni siku muhimu zaidi katika Ajenda ya Uzalishaji Mali katika Kaunti ya Kitui. Hivyo ndivyo mataifa ya Asia yalianza kukua hadi yakaipiku Kenya na mataifa mengine katika sekta ya uzalishaji bidhaa,” Bi Ngilu akasema.

Alimpongeza Rais Kenyatta akisema agizo lake kwamba sare za maafisa wa utawala katika serikali ya kitaifa zitengenezwe Kitui ni ishara kwamba anaunga mkono mradi huo- wa kwanza kuanzishwa na serikali ya kaunti nchini Kenya.

Hatua hii, akasema Bi Ngilu, inaambatana na nguzo ya Uzalishaji katika Ajenda Nne Kuu ya Maendeleo ya Rais Kenyatta ambayo inalenga kuchochea maendeleo kote nchini.

“Tulianza mwaka mmoja uliopita na tayari tumethibitisha kwamba tunaweza. Katika siku zijazo tutasaka zabuni ya kutengeneza sare nyingi za wafungwa na maafisa wa magereza,” Bi Ngilu akawaambia wanahabari katika kiwanda hicho.

Mavazi hayo yanatarajiwa kusambazwa kwa maafisa wa utawala katika sehemu mbalimbali nchini.

“Ndoto ya kaunti ya Kitui ya kuwa kitovu cha utengenezaji bidhaa imetimia. Tunazialika shule, hospitali, hoteli na asasi mbalimbali nchini kutupa zabuni ya kuzitengenezea sare za wafanyakazi wao,” akasema Bi Ngilu.