Kiwanda cha Kibos hatarini kufungwa
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI itafunga kiwanda cha Sukari cha Kibos ikiwa itabainika kuwa kinaelekeza uchafu katika mto Kibos ambao ni mmojawapo wa mito ambayo huelekeza maji katika Ziwa Victoria.
Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko Alhamisi aliwaambia wabunge kwamba sheria ya mazingira sharti izingatiwe na viwanda vyote ambavyo vimepewa leseni ya kuendesha shughuli zao humu nchini.
Aliwaambia wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Mazingira kwamba baada ya kupokea malalamishi kutoka kwa viongozi na wakazi wa eneo hilo, ameagiza Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) na maafisa kutoka wizara hiyo kuzuru kiwanda cha Kibos kuchunguza madai kwamba kinahatarisha maisha ya wakazi kwa kuchafua vianzo vya maji.
“Nimemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Nema Godfrey Wahungu kutuma maafisa wake huko kubaini ikiwa kiwanda hicho kinachafua mto Kibos. Vile vile, ningependa kuihakikishia kamati hii kwamba maafisa kutoka wizara yangu pia washiriki shughuli hiyo na malalamishi yakithibitishwa tutaamuru kufungwa kwa kiwanda hicho,” akasema.
“Sheria ni sheria na kampuni yoyote ambayo itahatarisha maisha ya maelfu ya wakazi kwa kuelekeza majitaka kwenye mito sharti iadhibiwe,” Bw Tobiko aliambia wanachama wa kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Maara Kareke Mbiuki.
Suala hilo liliibuliwa katika kamati hiyo na Mbunge Mwakilishi wa Kisumu Bi Rosa Akinyi Buyu ambaye alisema wakazi wa eneo la Kibos wamekuwa wakilalamika kuwa kiwanda hicho kinachafua mto ambao wao hutegemea kama chanzo cha maji.
“Maji ya mto Kibos pia hutumiwa na mifugo wa eneo hilo. Kwa hivyo, uchafu kutoka kiwanda hicho huhatarisha uhai wa mimea na wanyama,” akasema Bi Buyu.
Mbunge huyo alisema kuwa kampuni zote zinazoendesha shughuli zao katika eneo hilo sharti zikome kuhatarisha maisha ya wakazi.
Lakini Bi Buyu alimtaka Bw Tobiko kutofunga kiwanda hicho ikiwa uchunguzi utabaini kuwa kiwanda hicho kimetilia maanani malalamishi ya wakazi na kukoma kuelekeza uchafu ndani yam to Kibos.