Habari Mseto

Kiwanda cha mananasi kujengwa Gatundu Kaskazini

September 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

SERIKALI ya Kaunti ya Kiambu ina mpango wa kujenga kiwanda cha mananasi katika eneo la Gatundu Kaskazini.

Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema kuna haja ya kujenga kiwanda hicho kwa sababu wakazi wengi eneo hilo wanapanda minanasi kwa ajili ya kuzalisha mananasi.

“Iwapo kiwanda hicho kitajengwa wakazi wa eneo hilo watafaidika pakubwa kiuchumi, na pia vijana wengi watanufaika na kupata ajira,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema kwa muda wa miezi mitatu ijayo kaunti hiyo ya Kiambu itafanya utafiti ili kubainisha eneo faafu panapohitajika kujengwa kiwanda cha mananasi.

“Tunaelewa vyema wakazi wa hapa ni wakulima halisi kwa sababu mazao yanayopatikana katika eneo hili ni chai na mananasi. Kwa hivyo, ni vyema kufanya mpango jinsi wakulima wa huku wanavyoweza kufaidika na kilimo,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema hata wafugaji wa ng’ombe watasaidiwa kupata soko la maziwa yao.

“Hatutaki kuona wakulima wakiwa na shida na mazao yao. Kwa hivyo, kaunti itajitolea kuona ya kwamba kila mkulima anafurahia jasho lake,” alisema gavana huyo.

Alisema kaunti ya Kiambu ina mikakati kuona ya kwamba watu wanaoedesha Jujakali wanatafutiwa sehemu bora ya kuendesha kazi hiyo.

Alisema ofisi yake itafanya mikakati kuona ya kwamba sura ya Kiambu inabadilika na kuwa mahali pa kutamanika na wote.

“Muda uliosalia ni miaka miwili na kwa hivyo wakati huu tuko mbioni kuona ya kwamba tunatendea wananchi haki. Sisi hatuna nafasi ya kupiga siasa, bali ni kazi pekee,” alisema Dkt Nyoro.

Alisema miradi yote iliyopangwa kukamilika itashughulikiwa ipasavyo.

Alisema wafanyabiashara watapewa nafasi kuendesha shughuli zao bila kuhangaishwa.

“Kila mfanyabiashara ana haki ya kuendesha mambo yake bila kusumbuliwa. Ninawahakikishia kuwa hakuna yeyote atawahangaisha nikiwepo,” alisema gavana huyo.

Aliwahimiza wakazi wa eneo hilo washirikiane na wafanyakazi wa Kaunti ya Kiambu ili kusiwe na uhasama wa aina yoyote.