Kiwanda cha pamba chaiomba serikali kununua bidhaa zake
Na LAWRENCE ONGARO
KIWANDA cha nguo cha Thika Cloth Mills, kimeiomba serikali kuisaidia kwa kununua bidhaa zao ili kukinyanyua kibiashara.
Meneja mkuu wa kiwanda hicho Bw Dickson Kinuthia, alisema wanashirikiana na wakulima wa pamba wapatao 20,000 kote nchini ambao ndio wateja wao.
“Kiwanda cha Thika Cloth Mills, kinashikilia jukumu kubwa katika kilimo cha pamba na kwa hivyo ni muhimu kwa serikali kuwapiga jeki kwa kununua bishaa zao,” alisema Bw Kinuthia.
Alisema wakulima wanaokuza pamba wanatoka eneo la Mashariki, Pwani, Nyanza, na bonde la ufa. Pamba yote inayokuzwa huko huletwa katika kiwanda hiki ili kutengeneza nguo.
Alisema kiwanda hiki ndicho cha kipekee kinachounda nguo za jora ambazo zingine husafirishwa nje na zinginne hununuliwa hapa nchini.
Alisema shirika moja kutoka Ufaransa la French Development Agency AFD (Sunref) limeifadhili kiwanda hiki kwa kuleta mitambo mipya za kisasa kwa gharama ya Sh 170 milioni.
Ujumbe kutoka Ufaransa ulio ongozwa na Bw Raphael De Guerre ulitembea ndani ya kiwanda hicho na kujionea maendeleo yanayotekelezwa huko.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bi Tejal Dodhia, alisema miaka ya 80 na 90 kiwanda hicho kilikuwa mstari wa mbele kwa kutengeneza vitenge na nguo za watumishi wa serikali.
“Lakini baada ya uchumi kuanza kuzorota miaka ya 2000 kiwanda hiki kimepunguza utenda kazi wake. Hata hivyo bado tunajaribu kuwa katika soko tukifanya muhimu tunayoweza,” alisema Bi Dodhia.
Aliyasema hayo Jumatano wakati ujumbe wa kutoka Ufaransa ulipozuru kiwanda hicho ili kujionea wenyewe jinsi inaavyoendesha mambo yake ya kibiashara.
Alisema wanzidi kuendeleza baadhi ya ajenda nne za serikali ya maswala ya viwanda na kufanya juhudi kuajiri vijana ambao hawana kazi.
“Katika mashinani tumeajiri watu wapatao 54,000 ambapo tunatarajia wafike 10,000 baada ya miaka miwili zijazo,” alisema Bi Dodhia.
Aliwataka wananchi wa Kenya wawe mstari wa mbele kununua bidhaa kutoka hapa nchini ili kukuza uchumi wetu. Alisema wanaendeleza mwito wa ‘Jenga Kenya nunua Kenya’.