Habari Mseto

Kizimbani kwa kukwepa ushuru wa Sh97 milioni

January 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Mamlaka ya Kukusanya Ushuru nchini (KRA) ilimshtaki ajenti mmoja wa forodhani kwa kukwepa kulipa ushuru wa thamani ya zaidi ya Sh97 milioni.

Mshukiwa, Dickson Ogola, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Milimani Kennedy Cheruiyot Jumatatu kwa visa 12 vya kukataa kulipa ushuru.

Katika kisa cha kwanza, alishtakiwa kuepuka kulipa ushuru wa Sh60, 346,144 kinyume cha sheria ya forodhani.

Kulingana na mashtaka hayo, Bw Ogola na mtu mwingine walighushi stakabadhi za malipo mara 66 kati ya Januari 2012 na Agosti 2018 na kusababisha mamlaka hiyo kupoteza mapato.

Bw Ogola zaidi alikabiliwa na mashtaka 11 ya kudanganya katika matangazo forodhani kinyume cha sheria.

Maafisa hao walisababisha ushuru wa Sh36, 870,838 kupotea. Bw Ogola, alikuwa akitafutwa na KRA kwa miezi mitano na alikamatwa Jumamosi iliyopita Nairobi.