Habari Mseto

Kongamano la walimu lainua biashara baada ya Ramadhan

June 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

DOMINIC MAGARA na FARHIYA HUSSEIN

KONGAMANO la walimu wakuu na wasimamizi wa shule 7,500 za sekondari mjini Mombasa, kumeinua biashara hasa ya vyakula na mavazi.

Wageni hao ambao hutajwa kama watalii wa humu nchini, wamejumuika katika ukumbi wa shule ya mafunzo ya KRA eneo la Bamburi.

Nje ya ukumbi kuna hema zaidi ya 100 ambapo kunauzwa vyakula vya asili ya Kipwani pamoja na matunda, dawa na kanga.

Wachuuzi pia wanazunguka na bidhaa zao wakiuza simu, sanamu na saa za mkononi kati ya bidhaa nyingine.

Waliofika Mombasa kwa mara ya kwanza, walinunua suruali fupi za kuogelea na miwani za kujikinga na weupe wa mchanga wa bahari.

Hayo yamejiri huku wafanyabiashara wengine hasa katikati ya mji wa Mombasa wakilalamikia upungufu wa faida baada ya Ramadhan kukamilika.

Bi Biasha Sood alisema amehuzunika Ramadhan kumalizika kwani alikuwa akifanya biashara nzuri ya kuuza chakula nje ya soko la Mackinnon mjini Mombasa. Vyakula alivyokuwa akiuza ni mikate ya sinia, sambusa, mikate ya mayai, kababu na mikate ya mofa.

Mmiliki wa tuktuk, Bw Rashid Ali alisema walipata faida kubwa siku za Ramadhan pamoja na siku tatu za sikukuu ya Idd kwani walipata wateja wa kutosha.

Muuzaji matunda katika mkokoteni, Alfred Mumbo alisema: “Natamani sana kama kila siku ingelikuwa sawa na Ramadhan kwani biashara yangu ilikuwa nzuri sana. Natamani sikukuu ya Idd iwe ya siku nyingi kwani pia nimepata faida kubwa.”