Koros ashuku alitolewa kafara
Na LUCY KILALO
AFISA Mkuu Msimamizi wa Hospitali Kuu ya Kenyatta aliyetumwa kwa likizo ya lazima, ameelezea tashwishi kuhusu masaibu yaliyomwandama katika siku za hivi punde.
Bi Lily Koros Alhamisi aliambia Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Afya, kuwa matukio ambayo yamechafulia sifa hospitali ya Kenyatta yamefuatana kwa hali ambayo inaibua maswali, ingawa hawezi kubainisha iwapo kuna njama fiche.
“Sijui na sina hakina. Sitaki kusema hivyo kwa kuwa sina ushahidi,” alisema akijibu maswali ikiwa hatua yake ya kuwanyima tenda baadhi ya watu na kuzipeleka kwa mashirika ya serikali ndicho kiliwa kiini cha masaibu yake.
Baadhi ya tenda ambazo alifanyia mabadiliko ni za usambazaji maziwa, nyama na mafuta, ili kupunguza gharama. Tenda hizo alisema alizitoa kwa kampuni ya KCC, Kenya Meat Commission na National Oil.
Katika siku za hivi punde, hospitali hiyo imelazimika kutetea sifa yake huku ikikabiliwa na shutuma za mashini zake kutofanya kazi, madai ya unajisi wa wanawake waliojifungua, madai ya wizi wa mtoto, yote ambayo yamefanya utendakazi wa Bi Koros kumulikwa.
Bi Koros ambaye alikuwa amefika mbele ya kamati hiyo kufafanua ni vipi mgonjwa ambaye hakustahili alifanyiwa upasuaji, jana alieleza kamati ya bunge kuwa hana maelezo zaidi kwa kuwa alitumwa katika likizo wakati ambapo alikuwa akisubiri ripoti kutoka kwa waliohusika na upasuaji huo.
Hata hivyo, naibu wake, ambaye ni mkurugenzi wa huduma za matibabu, Dkt Benard Githae, aliambia kamati hiyo, kwamba hayo ni makosa yalitokea, na hayahusishi na njama yoyote.
Hayo yakijiri, Waziri wa Afya, Sicily Kariuki alikuwa mbele ya Kamati ya Seneti ya Afya, ambapo pia alikabiliwa na kipindi kigumu kuelezea kwa nini Bi Koros na Dkt Githae walipewa likizo ya lazima.
“Uchunguzi wa awali haumtaji afisa mkuu ama mkurugenzi wa huduma za matibabu. Ulimfuta kazi kwa sababu gani?aliuliza Seneta wa Trans Nzoia, Bw Mbito
Lakini waziri alisema kuwa wawili hao hawajafutwa kazi na kwamba walipewa likizo kuambatana na utaratibu wa masuala ya wafanyakazi ya KNH.
“Kulikuwa na kilio kutoka kwa umma na tulihitaji kupatia umma hatua ta dharura kuweka imani,” alisema akipuuzilia mbali madai kuwa wawili hao walifutwa ama kusimamishwa kazi.
Hata hivyo, waziri alielezea kuwa ripoti kutoka wa bodi simamizi ya hospitali ilionyesha kuwa tatizo la wagonjwa kutowekwa vibandiko vya majina yao kulichangia tukio hilo la upasuaji. Vile vile, ripoti hiyo na hata Dkt Githae waliambia kamati husika kuwa utaratibu kabla ya upasuaji wa kubainisha masuala kadha haukuzingatiwa.