Korti yakataa rufaa ya mzee aliyefungwa maisha kwa 'kunajisi bintiye'
Na MAUREEN KAKAH
MATUMAINI ya kuachiliwa huru kwa mwanamume aliyefungwa jela kwa “kusingiziwa” kunajisi binti yake, yamedidimia baada ya Mahakama ya Rufaa kukataa ushahidi mpya wa msichana huyo.
Bw Julius Musyoki Wambua aliwasilisha rufaa baada ya binti yake kufichua kwamba aliagizwa amsingizie makosa ya unajisi na mama yake alipokuwa na umri wa miaka 10.
Msichana huyo alifichua kwamba baba yake hakumdhulumu kimapenzi mbali ilikuwa njama ya mama yake aliyetaka afungwe jela.
Mzee huyo alifungwa jela maisha miaka minane iliyopita, na baada ya binti yake kufichua kilichotendeka alidhani alikuwa na sababu za kutosha kutia nguvu rufaa yake.
Hata hivyo, majaji William Ouko, Wanjiru Karanja na Jamila Mohamed walikataa kukubali ushahidi wa msichana huyo wakisema haukuwasilishwa kwa wakati unaofaa.
“Korti imeweka muda ambao rufaa inafaa kuwasilishwa na muda huo umepita,” majaji waliamua.
Bw Wambua alikuwa ameomba mahakama kuzingatia ushahidi wa binti yake ambaye alikuwa shahidi mkuu katika kesi yake alipofungwa.
Ingawa hatua ya binti yake ilionekana kama ambayo ingemuokoa aachiliwe huru, mtoto wake mwingine aliyetoa ushahidi dhidi yake akisema alimuona akitekeleza kitendo hicho hajakana ushahidi wake.
Mawakili wake Cyrus Maweu na Mike Mwema waliomba mahakama ichukulie ushahidi huo kama uliotolewa kwa nia mbaya. Hata hivyo, upande wa mashtaka ulipinga na kuomba majaji waukatae.
Upande wa mashtaka ulisema iwapo ombi la Bw Wambua lingezingatiwa, lingefungua mlango watu wawe wakibadilisha ushahidi baada ya kesi kufungwa.
Bw Wambua anazuiliwa katika Gereza la Kamiti akitumikia hukumu ya maisha gerezani.
Akihojiwa na runinga ya Citizen mwezi Machi, Bw Wambua alisema alisingiziwa mashtaka na mkewe waliyeachana kufuatia mzozo wa shamba.
Ingawa majaji wa mahakama ya rufaa walikataa ushahidi mpya wa binti yake, mahakama itaamua Septemba 27 iwapo itachunguza kesi ya Wambua.
Kwenye ripoti ya Citizen, bintiye Bw Wambua aliangua kilio akisema anajuta sana kutumiwa na mama yake kumweka baba yake kwenye mateso.
Alisema jambo hilo linamuumiza moyoni kupindukia na angetaka kuona baba yake ameachiliwa kutoka gerezani.
Matumaini yake sasa yanaweza kutokana na Rais Uhuru Kenyatta akiamua kumuachilia huru kwa kigezo cha huruma.
Visa vya wanaume kusingizwa kunajisi vimeongezeka maeneo mengi ya nchi.