Korti yaongeza kitita cha pesa kwa familia ya aliyeuawa kwa kupigwa na stima
KAMPUNI ya umeme nchini (KP), imeagizwa kufidia familia moja zaidi ya Sh3.2 milioni baada ya mahakama kubaini kampuni hiyo ilihusika na ajali iliyosababisha kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 56.
Jaji wa Mahakama Kuu Julius Ng’arng’ar alisema kuwa Leonard Chuphi Nguta, alidhihirisha kuwa alilipa bili kubwa za matibabu na gharama nyinginezo katika kumtibu na kumzika marehemu, ambaye alichomwa na umeme alipokuwa akirejea nyumbani kutoka shambani kwake.
Jaji huyo alitupilia mbali uamuzi wa awali wa mahakama uliomlipa Bw Nguta fidia maalum ya Sh657,500 na badala yake akamtunuku Sh3 milioni.
“Kwa hivyo, mlalamishi amefidiwa Sh3.2milioni. Amri za riba na gharama zilizotolewa na mahakama hapo awali zitabakia hivyo,” alisema jaji.
Fidia hii ilijumuisha Sh50,000 kwa maumivu na mateso na Sh100,000 kwa kupoteza matarajio ya maisha.
Mahakama pia ilisema kwamba stakabadhi zilizowasilishwa kwake zilionyesha kuwa Bw Nguta alitumia Sh2.4 milioni za gharama za matibabu kwa Kwekwe Ngute Choga.
“Mahakama hii, kwa hivyo, inaona kuwa pamoja na Sh657,500 alizotunukiwa, Bw Nguta pia ana haki ya kupata Sh2.4 milioni zilitumika kama bili za matibabu,” alisema jaji.
Bw Nguta aliwasilisha kesi hii kwa niaba ya Bi Choga, ambaye alichomwa na umeme mwaka wa 2020. Kisa hicho kilitokea Januari 15, 2020, marehemu alipokuwa akirejea nyumbani kutoka shambani.
“Aliingia kwenye dimbwi la maji lililokuwa limeangukiwa na nyaya za stima. Alinaswa na umeme na kupata asilimia 73 ya majeraha ya moto,” mahakama ilisikiza.
Mama huyo wa watoto watano alifariki wiki mbili baadaye alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Mombasa, ambapo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
“Ajali hiyo ilisababishwa na uzembe wa wafanyakazi, au maajenti wa KP ambao walikosa kuondoa waya uliokuwa umeanguka na kuwa chini kwa siku tatu,” Bw Nguta alisema kwenye stakabadhi za mahakama.
Bw Nguta aliomba kufidiwa Sh3 milioni, gharama za mazishi Sh656,000, na bili za matibabu za Sh2.4 milioni.
Kampuni hiyo hata hivyo ilikanusha kuhusika na ajali hiyo iliyosababisha kifo cha Bi Choga.
KP badala yake ilisema kuwa tukio hilo lilisababishwa na uzembe wa marehemu kwa kushindwa kuchukua tahadhari za usalama.
“Marehemu alishindwa kuzingatia hatua za usalama katika mazingira hayo, alipuuza hatari na ishara za onyo zilizowekwa na kampuni, na kuingilia waya za usambazaji wa umeme,” ilisema KP.
Kampuni hiyo pia ilimlaumu marehemu kwa kusimama karibu na nyaya za umeme bila kujali kabisa hatari iliyokuwa ikimkodolea macho na kuharibu nyaya zake za umeme.
Mahakama ambayo ilisikiliza kesi hii awali, ilibaini kuwa uzembe wa KP ulichangia ajali hiyo na kuiamrisha ilipe Bw Nguta Sh650,000 na Sh657,000 kama fidia ya jumla na maalum, mtawalia.
Hata hivyo, Bw Nguta hakuridhishwa na uamuzi huo na kukata rufaa katika Mahakama Kuu, akilalamika kwamba kiasi alichofidiwa kilikuwa kidogo mno licha ya ushahidi alioutoa kueleza gharama alizotumia kumtibu marehemu.
Jaji Ng’arng’ar alikubaliana na Bw Nguta, akibainisha kuwa alikuwa ametoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha gharama alizotumia akijaribu kuokoa maisha ya marehemu.