Habari Mseto

KQ kuwalipia Wakenya nauli kutoka New York hadi Nairobi

March 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

SHIRIKA la Ndege la Kenya Airways (KQ) limetoa tiketi za bure kwa Wakenya waliotaka kusafiri kutoka jijini New York, Amerika, hadi Nairobi, siku moja kabla ya serikali kuanza kutekeleza marufuku dhidi ya ndege za abiria kutoka nje.

Kwenye ujumbe katika akaunti yake ya Twitter, shirika hilo limesisitiza kuwa Wakenya hao wote watafanyiwa uchunguzi kuhusu maambukizi ya virusi vya corona watakapawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), Nairobi.

Wakenya hao pia watalazimika kujitenga katika mikahawa ambayo imeidhinishwa na serikali, kulingana na maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe mnamo Jumapili jioni.

“Ndege yetu ya mwisho kutoka uwanja wa JFK inaondoka leo na tunatoa tiketi za bure hadi Nairobi kwa Wakenya wenye haja. Kwa habari zaidi, wasiliana na maafisa wetu kwa nambari +1(866)5369224,” ikasema Jumanne.

Ikaongeza: “Zingatia kwamba abiria wote watachunguzwa kwa mujibu wa mwongozo uliowekwa na Wizara ya Afya. Tutanawiri tena na kuwahudumia kwa mara nyingine tutakaporejelea huduma zetu. Muwe salama.”

Tangazo la shirika hilo ni afueni kwa Wakenya ambao walikuwa wamepanga kurejea nyumbani kwani itawaokolea nauli kiasi cha Sh98,825.

Jumatano, Kenya Airways inatarajiwa kusimamisha “kwa muda” safari zote za kimataifa kama hatua ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Hii ni baada ya kubainika kuwa watu wote 16 wa mwanzo waliogunduliwa kuwa na virusi hivyo ni raia wa kigeni na Wakenya waliowasili nchini kutoka mataifa ya nje ambako visa vya ugonjwa wa Covid-19 vimeripotiwa.

Leo Jumanne waziri Kagwe ametangaza visa tisa mpya vya maambukizi na kufanya idadi ya wagonjwa wa Covid-19 kuwa 25 nchini.