KRA yalemewa na Google kortini kuhusu udukuzi wa mitambo
Na BERNARDINE MUTANU
Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru (KRA) imepoteza kesi dhidi ya Google, kuitaka kampuni hiyo kufichua mtu aliyedukua mfumo wake wa komputa hatua iliyopelekea mamlaka hiyo kupoteza habari muhimu.
Jaji wa Mahakama Kuu Pauline Nyamweya Jumanne alibatilisha agizo ambalo KRA ilipata kutoka kwa mahakama ya chini Januari kwa kusema agizo hilo halikufaa kwa kusema Google Kenya na Google Inc ni tofauti.
KRA ilikuwa imewasilisha Google Inc kama mshatikiwa katika kesi hiyo. Uamuzi huo ni pigo kubwa kwa KRA ikizingatiwa kuwa Google Inc, ambayo inasimamia akaunti ya gmail iliyotumiwa kuingilia mfumo huo, ina makao yake Marekani.
Kesi hiyo iliwasilishwa baada ya mwanamume wa miaka 28, Alex Mutungi Mutuku na wengine 11 kuingilia mfumo wa KRA hatua iliyopelekea kupotea kwa Sh3.9 bilioni.
Kuhusiana na kesi ya Bw Mutuku, waendeshaji wa mashtaka walisema kuwa washukiwa walitumia vifaa vilivyo na uwezo mkubwa na programu za kompyuta kuibia KRA karibu Sh4 bilioni.
Wengine ni Calvin Otieno Ogalo, Albert Komen Kipkechem, David Ndung’u Wambugu, Lucy Katilo Wamwandu, Edward Kiprop Langat, Kenneth Opege Riaga, Omar Ibrahim, James Mwaniki Gakung’u, Gilbert Kiptala Kipkechem na Joseph Kirai Mwangi.
Lakini walikana kuingilia mfumo huo kati ya Machi 2015 na Machi 2017.