Habari Mseto

KRA yamulika wafanyabiashara wa mitandaoni

May 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) imetaka wafanyabiashara wanaondesha shughuli zao mitandaoni kulipa ushuru ikionya baadhi yao wanaokwepa kwamba wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

“KRA imebaini kuwa baadhi ya watu wanaoendesha biashara mitandaoni huwa hawalipi ushuru wala kujaza fomu za kuonyesha ushuru wanaolipa kwa mapato yao kila mwaka. Watu hawa sharti walipe ushuru la sivyo wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria,” mamlaka hiyo ikasema kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Alhamisi.

Adhabu ya kutowasilisha taarifa ya ulipaji ushuru ni Sh20,000 kwa mwaka.

KRA ilisema wafanyabiashara mitandaoni wanahitajika kuwasilisha fomu za ushuru na kulipa ushuru zote ikiwemo ile ya ziada ya thamani (VAT), ushuru wa kampuni, ushuru za bidhaa kati ya aina zingine zinazolipwa na wafanyabiashara wa kawaida.

“KRA inashauri kwamba ni wale ambao wako katika tapo la wanaosamehewa ushuru, kulingana na sheria, ndio watasazwa,” ikasema taarifa hiyo iliyochapishwa magazetini.

Wale wafanyabiashara ambao hupata faida ya Sh5 milioni kwenda juu kila mwaka wanafaa kujisajili ili waruhusiwa kulipa VAT baada ya mwaka. Na wale ambao hupata faida isiyozidi Sh5 milioni wanafaa kulipwa ushuru wa awali (presumptive taxes).

KRA inataraji kwamba zaidi ya walipa ushuru 4 milioni watawasilisha taarifa zao za ulipaji ushuru (tax returns) kwa mfumo wa iTax kufikia Juni 30, 2019.

Mwaka 2018 zaidi ya walipa ushuru 3.2 milioni waliwasilisha taarifa zao za ulipaji ushuru kwa mfumo huo wa kimtandao.