Habari Mseto

Krismasi: Hali ya usalama yaimarishwa Pwani

December 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

SIAGO CECE na WINNIE ATIENO

SERIKALI imezidi kuimarisha usalama katika eneo la Pwani wakati huu wa msimu wa likizo ya sherehe za Krismasi.

Mshirikishi wa eneo la Pwani John Elungata alisema maafisa wa usalama wamewekwa katika maeneo tofauti tofauti na kuwa makini.

Bw Elungata pia alisema kutokana na operesheni za kuwanasa wahalifu mitaani tayari vijana zaidi ya 3,000 wameshikwa na kutiwa mbaroni kwa kujihusisha na ugaidi.

“Tumehakikisha kuwa kuna vikosi kadhaa na kuongeza usalama kwa sababu ya wageni ambao wanatarajiwa eneo hili msimu huu,” alisema Bw Elungata.

Pia, alisema vikosi tofauti vimetumwa hasa maeneo ya kuchoma makaa ya mikoko, maeneo ya kutengeza pombe ya Chang’aa na yale ya kuuza dawa za kulevya kwa sababu maeneo haya ndiyo yanafanya wakazi kuhofia usalama wao.

Aidha, Bw Elungata alisema raia sasa wamekubali kufanya kazi na afisa wa usalama, jambo ambalo limewasaidia kunasa washukiwa wa ugaidi hasa eneo la kata ndogo ya Kisauni.

Juhudi hizo zinafanyika wakati hoteli mbali mbali zinajitayarisha kwa likizo ya Krismasi huku asilimia 80 ya vyumba vyao vikiwa vimehifadhiwa.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Kufanya Kazi Pwani Husnain Noorani alisema eneo la Pwani limezidi kuimarika kutokana na miradi mbali mbali na miundo msingi iliyoboresha sekta ya utalii.

Meneja wa hoteli ya Pride Inn Flamingo Victor Shitakah kwa upande wake alisema kuwepo kwa safari nyingi za ndege zinazokuja maeneo ya Mombasa, Lamu na Malindi pia kumesaidia idadi ya wageni na watalii kuongezeka.

Eneo la Pwani linajulikana kupata watalii wengi hasa mwezi wa Desemba ambapo familia na wafanyi biashara wanakuja ufuoni kujivinjari.

Wikendi, Waziri wa Utalii Najib Balala aliitaja miradi ya kitalii ya kuvutia watalii ikiwemo bustani ya Mama Ngina iliyokarabitiwa kwa ghamara ya Sh460 milioni na kituo maalum cha kimataifa cha meli za kutalii kutia nanga iliyoko bandarini Mombasa kuwa miongoni mwa yanayotegemewa kuinua utalii Mombasa.

Kituo hicho kinatarajiwa kufunguliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mwezi huu, iligharimu Sh350 milioni ili kuimarisha utalii wa safari za meli na biashara bandarini.

Bw Balala alisema serikali imewekeza katika vituo hivyo vya kitalii huku akiwataka wawekezaji wa sekta hiyo kutafuta soko na kuziuza ughaibuni.

“Mnamo mwezi wa Oktoba, serikali iliweza kukamilisha ahadi ya ukarabati wa bustani ya Mama Ngina na sasa tumebakisha kutimiza ahadi yetu ya kukuza utalii wa meli kwa kufungua rasmi kituo hiki ambacho ni sawia na uwanja wa ndege,” alisema.

Bw Balala alisema utalii ni uti wa mgongo wa taifa hili ndiposa serikali imetilia mkazo sekta hiyo muhimu.

Akiongea kwenye sherehe za kuwatuza wafanyibishara huko Mombasa katika bustani la Mama Ngina, Bw Balala alisema kuimarishwa kwa miradi ya maendeleo hususan barabara kumechangia pakubwa katika kuimarisha sekta ya utalii.

Kulingana na Bw Balala miradi hiyo ya maendeleo itapanua uchumi wa eneo la Pwani.Alisema utalii umeimarika kwa asilimia 37 nchini huku watalii wakijaza hoteli za Pwani kwa asilimia 80.

Kwa upande wake, mwekezaji wa sekta ya utalii Bw Hasnain Noorani alisema utalii unanawiri nchini huku akiipongeza serikali kwa kuwekeza katika miradi ya kuinua sekta hiyo.