KRISMASI: Hofu wasichana wakijikeketa wenyewe
Na OSCAR KAKAI
HUHU shamrashamra za Krismasi zikinoga, imefichuka kuna watoto wanaobalehe katika Kaunti ya Pokot Magharibi ambao wameamua kujikeketa wenyewe baada ya wakeketaji wakongwe kuachana na mila hiyo iliyopigwa marufuku.
Mashirika yanayohusika katika kupambana na ukeketaji yamesema unyanyapaa unaelekeza wasichana kwa hatua hiyo hatari.
Mamia ya wasichana wenye umri mdogo katika kaunti hiyo huwa wako hatarini kukeketwa, kuozwa na kushika mimba wakati huu wa likizo.
Mashirika husika yamelalamikia ongezeko la visa hivyo na kusema asilimia 75 ya wasichana wako hatarini.
Wakiongea na Taifa Leo, baadhi ya wasichana kutoka Wadi ya Lomut ambao hawakutaka majina yao kutajwa walisema kuwa kutokana na msukumo kutoka kwa wasichana wenzao waliokeketwa kisiri, pamoja na wavulana wenye umri wao ambao hawaheshimu wale wasiokeketwa, waliamua kujikeketa kama njia ya kutimiza mila.
Walisema baadhi ya wakeketaji wameshikwa na kufungwa baada ya kufanya ukeketaji na wakahofia kuwa watanaswa wakitekeleza maovu hayo.
Mashirika ya kijamii katika kaunti hiyo walisema wanafahamu kuhusu matukio kama hayo na bodi ya kupigana na ukeketaji imeombwa kukabiliana na matukio yanayochipuka kama hayo.
Mratibu wa wakfu wa “I Rep”, Bi Domtilla Chesang alisema serikali inafaa kubadilisha mbinu zake na kutafuta sababu ya wasichana kujikeketa.
Alisema sheria haiongelei popote ikiwa wasichana watachukuliwa hatua wakijikeketa.