Habari Mseto

Krismasi: Mashoga na wasagaji kuandaa karamu Nairobi

December 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

WAPENZI wa jinsia moja wameamua hawataachwa nyuma katika sherehe za Krismasi mwaka huu.

Mashoga na wasagaji jijini Nairobi wameandaa karamu itakayofanyika kesho ambayo imeandaliwa na shirika la Afra-Kenya ambalo huwaleta pamoja wapenzi wa jinsia moja.

“Tutafungua kituo chetu kwa wale watakaokuwa Nairobi. Hafla hii itakuwa ya kifamilia kwa hivyo kuweni huru kuja na jamaa zenu,” ikasema sehemu ya mwaliko kutoka kwa shirika hilo, uliochapishwa katika mitandao ya kijamii.

Kinaya ni kwamba, Krismasi ni sherehe ya Kikristo, dini ambayo wakati mwingi huwa mstari wa mbele kukemea ushoga na usagaji.

Ushoga na usagaji huwa ni hatia Kenya, na anayepatikana na kosa hilo huweza kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 14 gerezani.

Kwa msingi huu, wengi walio katika makundi hayo huwa wanafanya shughuli zao kisiri wakihofia kuadhibiwa, kubaguliwa au kudhulumiwa katika jamii.

Baadhi waliotoa maoni yao kuhusu mwaliko huo, walisema utawapa nafasi kufurahia sawa na Wakenya wengine watakaokuwa wakisherehekea kwani “watakuwa pamoja na watu wanaoelewa mienendo yao”.