Habari Mseto

KRISMASI: Mbuzi kwa wateja 1,000, kila mfanyakazi kutuzwa Sh10,000

November 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA FAUSTINE NGILA

KAMPUNI ya uuzaji wa ardhi na mashamba Username Investments Ltd imetangaza kuwashukuru wateja na wafanyakazi wake katika msimu huu wa Krismasi kwa njia ya kipekee.

Katika sherehe ya ufunguzi wa ofisi mpya katika orofa ya nne, jumba la Le’Mac mtaani Westlands, afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo ametangaza kutuza zaidi ya wateja 1,000 mbuzi wa sikukuu huku wafanyakazi wakipata Sh10,000 kila mmoja.

“Kila mteja atakayenunua ardhi nasi au kukamilisha malipo ya ardhi yake kati ya Novemba na Desemba 31 atapata mbuzi wa thamani ya Sh5,000,” akasema.

Washindi wataingia kwa droo ya Januari mwaka ujao ambapo washindi watatu watajizolea likizo iliyolipiwa ya kusafiri nchini Thailand, jijini Mombasa na mbuga ya Maasai Mara.

Kampuni hiyo ilihama kutoka jumba la Mirage Towers, Westlands ili kuwahudumia wateja wake kwa njia murua zaidi, katika eneo linaloweza kufikika kwa urahisi.

Mwaka uliopita, Anne Lagat alijishindia likizo ya Dubai, James Omari akasafiri Mombasa huku Ronald Maathai akijivinjari mbugani Maasai Mara.

Bw Julius Karanja ambaye ndiye mkuu wa uhasibu alirai wasimamizi wa kampuni kuwapa wateja na wafanyakazi kipa umbele na kukoma kuweka faida mbele.

“Hapa Username, tunajizatiti kubadilisha Maisha ya Wakenya wa kipato cha chini ambao wana ari ya kumiliki ardhi,” akasema.

Kampuni hiyo imejizolea sifa ya kuwapa wateja ardhi kwa bei nafuu na katika mipango inayowafaa, bila kuwapunja.

Hulka hii imechangia pakubwa katika uzoaji wake wa tuzo mbalimbali katika sekta hiyo. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita pekee, Username imeshinda tuzo zaidi ya 20.

Afisa mkuu wa mauzo Bw Joseph Gitonga alisema hili limetokana na juhudi za kampuni hiyo ya kujenga imani miongoni mwa wateja, ambapo imetoa zaidi ya hatimiliki 6,000 kwa wateja.

Hii ni licha ya sekta ya ardhi nchini kukumbwa na wizi na utapeli wa kiwango cha juu uliopelekea maelfu ya Wakenya kupoteza mabilioni ya pesa wakifukuzia kumiliki ardhi.

“Licha ya changamoto hizi, tumejitolea kurejesha imani hii iliyopotea miongoni mwa Wakenya kwa kuwahakikishia huduma za kikweli,” akasema Bw Gitonga.