KRISMASI: Serikali kulipa madeni ya wanakandarasi
Na CHARLES WASONGA
KAIMU Waziri wa Fedha Ukur Yatani ametoa hakikisho kwamba Serikali ya Kitaifa imejitolea kulipa madeni inayodaiwa na wanakandarasia na wafanyabiashara.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumanne Bw Yatani alisema Serikali ya Kitaifa inadaiwa jumla ya Sh58.2 bilioni. Kati ya pesa hizo Sh43.2 bilioni ni madeni ambayo uhalali wayo unabishaniwa na ambayo yanafanyiwa ukaguzi na uchunguzi.
“Madeni halali ambayo Serikali Kuu inadaiwa na wafanyabiashara ni Sh15.0 bilioni. Na jumla ya Sh10.8 bilioni zimelipwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Serikali ya Kitaifa imeahidi kulipa Sh4.2 bilioni zilizosalia kufikia Januari 15, 2020,” akasema Bw Yatani.
Madeni ya kima cha Sh43.2 bilioni ambayo uhalali wayo unabishaniwa yamewasilisha kwa kamati maalum shirikishi (Multi Agency Team) ambayo Rais Uhuru Kenyatta aliamuru ubuniwe, alipoongoza mkutano wa baraza la mawaziri wiki jana.
Kulingana na Waziri Yatani, baadhi ya mashirika ya serikali kuu na serikali za kaunti zimekuwa zikidinda kulipia bidhaa na huduma inazopewa na sekta ya kibinafsi.
“Baadhi ya madeni madeni hayajalipwa kwa kipindi kirefu (wakati mwingine miaka mitano),” Bw Yatani akasema kwenye taarifa ambayo ilitoa hali halisi ya madeni ambayo hayajalipwa.
Akaongeza: “Hali hii imeathiri uchumi na kuchochea zaidi janga la ukosefu wa ajira na umasikini.”
Kuhusu serikali za kaunti, Waziri Yatani alisema kwa ujumla zinadaiwa Sh22.71 bilioni ambazo zimethibitishwa kuwa halali.
Ukaguzi maalum ambao ulifanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufikia Juni 30, 2018 unaonyesha kuwa serikali za kaunti zinadaiwa jumla ya Sh88.98 bilioni, ambapo Sh51.2 bilioni zimethibitishwa kuwa halali.
Hii ni kwa sababu madeni ya kima cha Sh37.7 bilioni zinakosa stakabadhi za kuonyesha kuwa bidhaa au huduma ziliwasilishwa au kazi ilifanywa. Na hivyo, hazijathibitishwa kulipwa.
“Madeni halali ambayo yamelipwa kufikia Desemba 18, 2019 ni Sh28.57 bilioni, hivyo Sh22.7 bilioni hazijalipwa,” akasema Yatani.
Kufikia Jumatatu Desemba 23 Hazina ya Kitaifa ilikuwa imetoa jumla ya Sh112.04 bilioni kama fedha za mgao wa fedha katika bajeti ya kitaifa.
“Kutolewa kwa mgao wa fedha za Desemba na miezi mingine kuanzia mwaka ujao kufanyika tu baadhi ya serikali za kaunti kuwasilisha taarifa ya ulipaji wa madeni, kulingana na utaratibu uliotolewa na Hazina ya Kitaifa na Masimamizi wa Bajeti (CoB),” akasema Yatani.