Habari Mseto

Krismasi ya kipekee kwa kina mama tisa waliojifungua Sikukuu

Na KNA December 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

ILIKUWA Krismasi ya aina yake kwa kina mama ambao walipata watoto tisa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Bungoma katika siku ya Wakristo kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu.

Baadhi ya wanawake wameripoti kuwa walitarajia kujifungua siku tofauti na Desemba 25.

“Siku ya leo nina furaha sana. Ninamuona huyu mtoto kuwa zawadi kwangu kwa sababu nilitarajia azaliwe tarehe 31 lakini Mungu akatenda ishara akazaliwa siku ya Krismasi,” akasema Bi Aisha.

Bi Elizabeth Olengo ni mmoja wa waliojifungua salama na anashukuru usimamizi wa hospitali kwa kuwezesha apate baraka ya Krismasi.

Kulingana na usimamizi wa hospitali hiyo, wanawake sita kati yao walizaliwa kwa njia ya kawaida huku watatu wakizaliwa kwa njia ya upasuaji.

“Kama hospitali, tunaweka mikakati ili tuone ya kwamba tunaweza kusherehekea na watoto hawa ambao tunawaita Emmanuel,” akasema Mwuguzi Mkuu Joshua Matepu.

Wazazi waliojifungua walidhihirisha furaha yao wakisema ni fursa maalumu kwao kujifungua siku ambayo Wakristo wanaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu.