Habari MsetoMichezo

KSCE 2019: Wanafunzi wanaspoti wang'aa

December 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WANYORO

WANAFUNZI wa Shule ya wavulana ya Kangaru, Embu ambao walikuwa viranja na waling’aa kwenye fani ya spoti, ni kati ya watahiniwa waliofanya vizuri katika Mtihani wa KCSE ulitolewa Jumatano na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha.

Mchezaji mahiri wa raga Muchina Peter Kariuki ambaye aling’aa kwenye michezo ya Afrika Mashariki na Kati, alipata A- huku nyota yake ikipaa zaidi baada ya kufanya vyema katika masomo ya hesabati na Sayansi.

Mwalimu Mkuu Kiminda Wambugu alisema Bw Kariuki ambaye pia alikuwa kiranja wa shule hiyo, alikuwa kati ya wanamichezo wengine walioongoza kwa mfano mwema na kuipa shule hiyo sifa kwa kufanya vyema.

Bw Kariuki ambaye analenga kuwa daktari, anatoka katika familia maskini na alikuwa kati ya wanafunzi walionufaika na ufadhili wa benki ya Equity maarufu kama ‘Wings to Fly’.

Bw Wambugu pia alimsifu mwanafunzi huyo kwa kuwa aliongoza shule yake kumaliza katika nafasi ya nne kwenye raga ya wachezaji 15 kila upande katika mashindano hayo ya shule za upili ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kati.

“Alikuwa mwanafunzi aliyeongoza timu vyema kutamba alipoingia uwanjani. Alikuwa mwanafunzi mwenye sifa zote nzuri na heshima kwa walimu wake,” akaongeza Bw Wambugu.

Wanafunzi wengine ambao walifanya vyema na walikuwa kwenye kikosi hicho cha raga ni Gichovu Godwin Munene na Lincoln Njagi Munene ambao walipata alama ya B.

Aidha Bw Wambugu alisema shule hiyo ina vifaa vya kushiriki michezo na mara nyingi huwashauri wanafunzi kuvitumia baada ya vipindi vya masomo.

“Baada ya vipindi darasani, wanafunzi huwa wanafanya mazoezi ya viungo wakiongozwa na walimu vijana. Viwanja vyetu huanda michezo ya kitaifa na kieneo na sisi huwatia wanafunzi wetu motisha ya kuvitumia vyema,” akaongeza.

Hadi wakati gazeti hili likichapishwa, ilikuwa imethibitishwa kwamba wanafunzi 15 walikuwa na alama A-. matokeo ambayo yalionyesha kwamba shule hiyo ilikuwa imefanya vyema kuliko mwaka jana.

“Mwaka jana tulikuwa wanafunzi watatu wenye A- lakini kwa sasa tumethibitisha 15 wamezoa alama hiyo na bado tunaendelea kutuma arafa. Tuna wingu la matumaini ya kupata matokeo mazuri,” akasema.