Habari Mseto

Kufunga TV zisionyeshe Raila akiapishwa kulikandamiza haki – LSK

March 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

CHAMA cha wanasheria nchini (LSK) kimeishtaki Serikali na kufufua kesi ya kufungwa kwa vituo vitatu vya runinga nchini na Serikali miezi miwili iliyopita.

Ijapokuwa Mahakama Kuu ilikuwa imeagiza vituo vya NTV , KTN News na Citizen vifunguliwe, chama cha LSK kimesema katika kesi kilichowasilisha kwamba haki zilikandamizwa.

Kupitia kwa wakili Daniel Musyoka , LSK  kimesema kwamba sheria imeizuia Serikali kuthibiti kituo chochote kile cha upeperushaji matangazo.

LSK kimemshtaki Waziri wa Usalama , Dkt Fred Matiang’I, Waziri wa Teknolojia ya Habari Bw Joe Mucheru na Mkurugenzi  wa Mamlaka ya Mawasiliano (CA) Francis Wangusi na Mwanasheria mkuu (AG).

Kwenye kesi hiyo LSK kimevitaja vituo vikuu vya habari kama waathiriwa wakuu.

Vituo hivi vilifungwa pasi kuarifiwa na Serikali kama inavyotakiwa kisheria.

LSK kimesema kwamba  Serikali ilikaidi maadili ya umma yanayokubalia umma kupashwa habari pasi kukandamizwa. Vituo vilifungwa siku saba mfululizo.

“Washtakiwa (Matiang’i, Wangusi na Mucheru) walitumia vibaya mamlaka yao kwa kufunga vituo hivi. Hadi waleo hawajatoa sababu ya  kuvizima,” akasema Musyoka.

Vituo hivi vilizimwa visionyeshe uapisho wa kinara wa Nasa Raila Odinga mnamo Januari 30, 2018.

Mamilioni ya wafuasi wa Nasa walifurika uwanja huo wakati Odinga aliapishwa.

Jaji Enoch Mwita atatoa uamuzi Mei 21, 2018.