• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Kuna fedha za kutosha kufadhili afya kwa Wakenya wote – Rais Kenyatta

Kuna fedha za kutosha kufadhili afya kwa Wakenya wote – Rais Kenyatta

Na CHARLES WASONGA 

RAIS Uhuru Kenyatta amesema kuna pesa za kutosha nchini kufadhili mpango wa afya kwa wote nchini ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo, kama inavyofanya kaunti ya Makueni.

Akiongea Jumanne alipokutana na wanachama wa Kamati ya Magavana kuhusu Afya katika Ikulu ya Nairobi, Rais alisema kile kinachohitajika na mageuzi kufanywa katika mfumo wa utoaji huduma za afya ili kuhakikisha manufaa yamewafikia watu wote.

“Afya kwa wote ni mojawapo ya ajenda nne nne kuu ambayo serikali yangu imeazimia kutekeleza ndani ya miaka mitano ijayo. Nashawishika kuwa kuna pesa za kutosha nchini kutekeleza mpango huu ambao utahitaji ushirikiano kati ya serikali kuu na serikali za kaunti na washirika wa kimataifa,” akasema Rais Kenyatta.

Mkutano huo ulihudhuriwa na magavana 11, akiwemo mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Magavana (CoG) kuhusu Afya Mohammed Kuti (Isiolo) na Naibu Mwenyekiti wa baraza hilo Bi Anne Waiguru (Kirinyaga).

Rais Kenyatta aliongeza kuwa kando na afya, ujenzi wa nyumba 500,000, usalama wa chakula na lishe bora, ustawi wa sekta ya utengenezaji bidhaa, ni ajenda zingine ambazo serikali yake inapania kutekeleza.

Kamati ndogo itakayoangalia masuala yote yanayohitajika kufanikisha azma ya kuafikiwa kwa afya kwa wote ilibuniwa katika kikao hicho. Kamati hiyo itaongozwa na Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki na Gavana Kuti.

Vile vile, kamati hiyo itasimamia majaribio ya utekelezaji wa mpango wa afya kwa wote katika kaunti chache kwa muda ambao utaafikiwa baadaye.

Mgavana wengine waliohudhuria mkutano huo katika Ikulu ni pamoja na; Charity Ngilu (Kitui), Kiraitu Murungi (Meru), Francis Kimemia (Nyandarua), kati ya wengine.

Tayari Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana  ameanza kutekeleza mpango wa afya kwa wote, mpango ambao umeshabikiwa na Wakenya wengi kwa sababu umeandikisha ufanisi mkubwa.

You can share this post!

Vinara wa NASA wakubaliana kuepuka siasa za 2022

Miguna Miguna sasa awaomba Wakenya wamchangie hela arudi...

adminleo