Habari Mseto

Kuna uwezekano wa mashambulizi ya kigiaidi Kenya, Amerika yaonya

February 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

SERIKALI ya Marekani imetoa tahathari kwa raia wake waliomo nchini Kenya katika miji ya Nairobi, Naivasha na Nanyuki, pamoja na miji ya Pwani kuwa wajitahathari kwani wanaweza kuvamiwa na magaidi.

Serikali hiyo imewataka raia wake wanaosafiri kuelekea Nairobi kujiingiza katika program ya kufuatilia usafiri wao, aidha kupitia intaneti ama kwenda katika makao ya ubalozi.

“Tunashauri raia wa US wanaosafiri kuelekea ama kuishi Nairobi kujiingiza katika idara ya ubalozi kwenye program ya Smart Traveler. Ikiwa huna intaneti, fika katika makao ya ubalozi,” idara ya ubalozi wa US Kenya ikasema Jumatatu.

Serikali hiyo iliendelea kuwakumbusha raia wake kuwa wanafaa kuwa waangalifu katika kila sehemu ya Kenya, haswa katika maeneo ya umma kama ya kununua, mahoteli na maeneo ya ibada.

Ujumbe huu unakuja wiki chache tu baada ya vamizi katika hoteli ya Dusit D2 mtaa wa Westlands wiki chache zilizopita, ambapo watu 21 waliaga dunia.

Mnamo Januari 25, serikali hiyo iliwataka Wakenya kuwa waangalifu wanapokuwa katika maeneo ya umma, mbali na kuwataka wageni kuwa na nakala zao za usafiri zikiwa katika hali nzuri kila wakati.