KUPUNGUZA AJALI: Serikali yaanza kupanua barabara Salgaa na Sachangwan
NA PETER MBURU
Wakazi wa maeneo ya Salgaa na Sachangwan wameipongeza serikali kwa kuanzisha ujenzi wa barabara pana katika eneo hilo lenye sifa mbaya ya ajali, wakisema utasaidia kumaliza ajali.
Kuanzia asubuhi ya Jumatatu, magari ya ujenzi yalianza kazi hiyo ya upanuzi wa barabara kati ya Sobea na Mau-Summit ambapo pamekuwa eneo la ajali kwa muda mrefu sasa.
Wakazi wa maeneo hayo, ambao wengi wao wameadhiriwa na ajali za mara kwa mara ambazo wameshuhudia kwenye barabara hiyo walihongera hatua ya serikali, wakisema itasaidia kupunguza ajali kwenye barabara hiyo.
“Tumekuwa tukishuhudia ajali nyingi mbaya kwenye barabara hii kwa miaka mingi na huwa tunahisi vibaya kuona watu wakiaga dunia kila mara. Tunashukuru kwani sasa huenda ajali zikazikwa kwenye kaburi la sahau,” akasema Bw Josephat Karanja, mkazi wa Sachangwan.
Kulingana na wakazi, upanuzi wa barabara hiyo ili kuwe na mipito miwili kutatoa suluhu ya kudumu na kumaliza visa vya ajali.
“Tunahofia na kuchukia ajali haswa misimu ya kusherehekea kwani ndipo tunawapoteza wakenya wengi. Kwa muda mrefu tumekuwa tukiiomba serikali kutatua jambo hilo, lakini sasa tunashukuru kwani imechukua hatua,” akasema Bi Lucy Wangari, mfanyabiashara eneo la Salgaa.
Wazo la kupanua barabara hiyo lilianzishwa mwanzoni mwa mwaka huu, baada ya ajali nyingi ndani ya kipindi cha miezi miwili, zilizowaangamiza Zaidi ya watu 100.
Serikali ilitangaza zabuni ya ujenzi huo na kampuni ya kutoka Uchina , China Railways No. 10 limited ikazawadiwa zabuni hiyo kwa Sh748milioni.
Ujenzi huo sasa utachukua kipindi cha mwaka mmoja, ukijumuisha urefu wa kutoka Sobea hadi Mau-Summit, kilomita 22.
Kulingana na naibu mkurugenzi wa mawasiliano katika mamlaka ya kusimamia barabara kuu nchini (KeNHA) Bw Charles Njogu, ujenzi huo aidha utahusisha kuwekwa kwa alama za kutahadharisha watumizi wa barabara na kituo cha kukagua breki za magari yanayopitia hapo.
Mengi ya magari yaliyofanya ajali katika barabara hiyo yalihusishwa na kufeli kwa breki.