Kuria ashangaa handisheki bado haimtoi kortini
RICHARD MUNGUTI na VALENTINE OBARA
MBUNGE wa Gatundu Kusini, Bw Moses Kuria ameshangaa kwamba kesi yake kuhusu uchochezi dhidi ya Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga ingali inaendelea licha ya kuwepo kwa handisheki.
Jana Bw Alexander Mathenge ambaye ni mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA) alifika katika Mahakama ya Milimani, Nairobi kutoa ushahidi dhidi ya mbunge huyu katika kesi hiyo inayohusu uchochezi na uhasama wa kijamii.
“Nilitumiwa video kutoka kwa DCI nikaagizwa kuchunguza mienendo ya Kuria na matamshi yake ambayo yaliaminika kuchochea ghasia za kijamii na kumtusi Raila. Nilikagua video yote nikatambua kwamba, kwa maoni yangu, Bw Kuria alikiuka sheria aliposema watu waliompigia Raila kura 70,000 eneo la Kati wasakwe, na wakazi wa eneo la Kati wasikubali kutolewa nyama mdomoni,” akasema Bw Mathenge.
Matamshi hayo yalidaiwa kutolewa katika eneo la Wangige, Kiambu wakati Bw Kuria alipohutubia umma mnamo Septemba 19 baada ya kuharamishwa kwa ushindi wa Rais Kenyatta na Mahakama ya Juu.
Upande wa mashtaka umefunga kesi na Bw Kuria atajitetea Juni 27, ambapo anatarajiwa kuomba korti imwachilie huru. Alikuwa amekanusha madai hayo na yuko nje kwa dhamana.
Awali Jumatatu, Bw Kuria alielekea kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook kueleza hisia zake kuhusu masaibu hayo yanayomkumba licha ya kuwepo muafaka kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, almaarufu handsheki.
“Mwaka mmoja na robo baada ya handsheki, narejea katika Mahakama ya Milimani itakayosikiliza kesi ambapo nimeshtakiwa kwa kumwambia Raila Odinga “wembe ni ule ule” kabla ya marejeo ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, 2017. Mungu nisaidie,” akasema, huku akijitaja kuwa ‘mfungwa wa mwisho wa kisiasa’.
Wakati Bw Odinga na Rais Kenyatta walipoweka muafaka wa maelewano mnamo Machi 9, 2018, taifa lilitazamia kusahau yaliyopita na hivyo basi huenda Bw Kuria naye alitarajia kesi hiyo ingeondolewa.
Kwenye ushahidi wake, Bw Mathenge alieleza mahakama jinsi Bw Kuria alivyotoa matamshi machafu tusiyoweza kuchapisha katika gazeti hili, dhidi ya Bw Odinga na mkewe Ida.
Video pia ilichezwa kortini upande wa mashtaka ukitaka kuthibitisha kuwa mbunge huyo alizua madai kwamba Bw Odinga alitoa watoto wake kafara na kamwe hawezi kuaminiwa na watoto wa Kenya akiwa rais.
Mapema Februari kesi hiyo iliposikilizwa, Inspekta Mkuu Kassim Baricha aliambia mahakama kwamba matamshi ya Bw Kuria yalikuwa na uwezo wa kusababisha taharuki nchini.
Bw Odinga alisusia uchaguzi wa marudio wa urais ambapo mgombea mwenza wake alikuwa ni Kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka chini ya Muungano wa NASA.
Uchaguzi huo wa marudio uliandaliwa baada ya Mahakama ya Juu ikiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga, kufutilia mbali ushindi wa Rais Kenyatta katika uchaguzi uliofanywa Agosti 2017, kwa msingi kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilikiuka sheria na hivyo kulazimu uchaguzi huo usiwe huru na wa haki.
Hatua ya Bw Odinga kususia uchaguzi ulimfanya Rais Kenyatta kuibuka mshindi tena, kwani hakuwa na upinzani mkali.